Ripota wa Al-Mayadeen: Utawala wa Kizayuni umeshindwa na Iran
(last modified Sat, 26 Oct 2024 11:26:55 GMT )
Oct 26, 2024 11:26 UTC
  • Ripota wa Al-Mayadeen: Utawala wa Kizayuni umeshindwa na Iran

Mwandishi wa kanali ya Al-Mayadeen aliyeko mjini Tehran ameashiria kushindwa utawala wa Kizayuni wa Israel na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuibuliwa mlingano mpya wa nguvu katika eneo.

Mwandishi wa kanali ya Al-Mayadeen aliyeko mjini Tehran ameripoti kuwa: Shambulio la alfajiri ya leo Jumamosi hapa mjini Tehran lililotekelezwa na utawala haramu wa Israel limemalizika kwa ushindi wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran na harakati za muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na harakati za muqawama zimeleta mlingano mpya katika eneo.
Ikiwa ni katika hatua zake za kudumisha ghasia na mvutano katika eneo, utawala wa Kizayuni umeshambulia vituo kadhaa vya kijeshi katika majimbo ya Tehran, Khuzestan (kusini magharibi mwa Iran) na Ilam magharibi mwa Iran.

Kwa mujibu wa tangazo la kitengo cha mahusiano ya umma cha kituo cha ulinzi wa anga cha Jamhuri ya Kiislamu, shambulio hilo limesababisha uharibifu mdogo katika vituo hivyo ambapo uchunguzi unaendelea kufanywa kubaini kiwango hasa cha uharibifu uliotokana na shambulio hilo la kichokozi.