Iran yatoa wito wa kufanyika juhudi zaidi za kurejesha amani Gaza, Lebanon
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametoa wito wa kuongezwa juhudi za kidiplomasia za kuleta amani huko Gaza na Lebanon.
Abbas Araghchi ameyasema hayo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Misri Badr Abdelatty siku ya Jumatatu.
Araghchi pia amesisitiza udharura wa kusitishwa mapigano katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu.
Ametoa wito wa kutumwa mara moja misaada ya kibinadamu kwa wakimbizi wa Gaza na Lebanon. Hali kadhalika Araghchi amesema watawala wa Israel wanalenga kupanua vita katika eneo lote la Asia Magharibi.
Ameongeza kuwa, Iran inataka usitishaji vita lakini wakati huo huo inahifadhi haki yake halali ya kujilinda dhidi ya uvamizi wowote wa Israel.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza haja ya kuchukuliwa hatua madhubuti katika kiwango cha kimataifa, haswa na ulimwengu wa Kiislamu, kwa shabaha ya kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya Wapalestina.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Badr Abdelatty, kwa upande wake, amesisitiza juu ya hitajio la kufanyika juhudi za kupunguza mivutano katika eneo.
Utawala haramu wa Israel ulianzisha kampeni yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 2023. Baadaye utawala huo ulipanua mashambulizi hadi Lebanon.
Tangu wakati huo, utawala haramu wa Israel umeua Wapalestina 43,370 wakati idadi ya waliouawa huko Lebanon inakadiriwa kuwa karibu 3,000. Aghalabu ya waliouawa shahidi katika mashambulizi hayo ya Israel ni wanawake na watoto.