Hizbullah ya Lebanon yazindua kituo cha makombora cha Emad 5
Hizbullah ya Lebanon imezindua picha za kituo cha makombora cha chini ya ardhi cha Emad 5.
Kwa mujibu wa kanali ya Sahab, sehemu ya kituo cha makombora cha Emad 5 kilicho chini ya ardhi kimeonyeshwa kwenye mkanda wa video uliotangazwa jana Jumapili tarehe 3 Novemba na Idara ya Habari za Vita ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon, Hizbullah.
Katika video hiyo, Shahidi Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah nchini Lebanon amesikika akisisitiza kuwa: "Hatutaondoka kwenye medani ya mapambano na wala hatutaweka chini silaha zetu."
Kituo cha makombora cha Emad 5 kimezinduliwa huku Hizbullah ikitangaza katika taarifa yake ya siku ya Jumapili kuwa muqawama wa Kiislamu umelenga kwa makombora kadhaa kambi maalumu yenye mafungamano na Jeshi la Wanahewa la Israel katika mji unaokaliwa kwa mabavu na Israel wa Haifa
Jumatatu tarehe 23 Septemba, jeshi katili la utawala wa Israel lilianzisha mashambulizi makubwa katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon, ambayo yangali yanaendelea hadi sasa. Hizbullah ya Lebanon pia imefanya oparesheni nyingi dhidi ya vituo vya kijeshi na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na utawala pandikizi wa Israel, ili kukabiliana na hatua ya utawala huo ya kuwalenga raia wa nchi hiyo, kwa kurusha mamia ya makombora katika maeneo ya utawala wa Kizayuni.