Lavrov: BRICS inataka kuisambaratisha nguvu ya sarafu ya dola
(last modified Mon, 04 Nov 2024 12:59:12 GMT )
Nov 04, 2024 12:59 UTC
  • Lavrov: BRICS inataka kuisambaratisha nguvu ya sarafu ya dola

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema kuwa kundi la BRICS linataka kuanzisha mifumo ya fedha mbadala na kupunguza utegemezi kwa sarafu ya dola.

Sergei Lavrov amesema katika mahojiano ya hivi karibuni na kanali ya kimataifa ya BRICS kuwa kitendo cha kutumia sarafu ya dola kama wenzo ni tisho kwa kwa amani duniani, na kundi la BRICSA linatafuta mifumo ya fedha mbadala ambayo itapunguza utegemezi kwa sarafu ya dola. 

 BRICS na mkakati wa kuacha kutegemea sarafu ya dola

Lavrov ameongeza kuwa, dola ya Marekani imekuwa silaha ya kudhibiti uchumi wa dunia, na BRICS inataka kuepuka hatari zilizopo kwa kuweka utaratibu wa malipo kwa kuzingatia sarafu za kitaifa. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia ameashiria kupanuka kwa kundi la BRICS hivi karibuni na kujiunga na kundi hilo nchi kama Iran, Saudi Arabia na Imarati na kusema: "Wanachama hawa wapya wamepelekea kuimarika nafasi ya BRICS kwa kuwa na itibari ya kimataifa."

Kuhusu Iran, Lavrov amesema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejiunga na kundi hilo kama nguvu muhimu ya kiuchumi na iliyo na mchango athirifu katika kuimarisha nafasi ya kundi hilo."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia pia ameashiria nafasi ya Marekani katika kuvuruga utendaji wa Shirika la Kimataifa la Biashara (WTO) na kuongeza kuwa: "WTO imeundwa ili kushughulikia hitilafu za kibiashara hata hivyo Marekani inakwamisha ufuatiliaji wa masuala kama ya ushuru usio wa kiadilifu n.k kwa kuzuia kuitishwa vikao vya shirika hilo."