Kuendelea jinai za magaidi Parachinar, Pakistan
(last modified Wed, 27 Nov 2024 02:25:45 GMT )
Nov 27, 2024 02:25 UTC
  • Kuendelea jinai za magaidi Parachinar, Pakistan

Baada ya shambulio la hivi majuzi la kigaidi dhidi ya Mashia wa Parachinar katika Wilaya ya Kurram nchini Pakistani, mamlaka za nchi hiyo zimeripoti uhalifu mwingine wa matakfiri dhidi ya Mashia wa Parachinar.

Kulingana na maafisa hao, baada ya shambulio la kigaidi la hivi majuzi karibu na mji wa Parachinar, makumi ya watu wengine pia wameuawa katika mashambulio mengine ya kikaumu katika eneo hilo.

Kwa mujibu wa polisi wa kieneo wa Pakistan, hali ya Parachinar bado ni ya machafuko, na katika siku mbili zilizopita, watu wasiopungua 37 waliuawa na wengine 30 walijeruhiwa katika mashambulizi yenye mielekeo na hisia za kimadhehebu ya matakfiri.

Licha ya kuwa, inasemekana kwamba, mauaji haya yalifanyika baada ya mvutano na mzozo kati ya makabila ya Alizai na Bagan katika eneo la Kurram karibu na mpaka wa Afghanistan, lakini hakuna shaka kwamba tofauti za kieneo na kikabila ni kisingizio tu cha matakfiri cha kuua Mashia wa Parachinar kwani kunaonekana mambo ya nje ya kikanda na nafasi ya vibaraka wenye mfungamano na Uzayuni katika kuunga mkono matakfiri katika kufanyika jinai hiyo. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, lengo lao ni kugeuza eneo hili kuwa Gaza au Myanmar nyingine katika ulimwengu wa Kiislamu.

Fauka ya hayo, matakfiri wenye mafungamano na ugaidi wa kimataifa kwa kushadidisha jinai zao huko Parachinar wanajaribu kupotosha fikra za umma duniani hususan Waislamu kuhusiana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.  Mji wa Parachinar ndio kitovu cha kabila la Kurram, ambalo wengi wao ni Mashia.

 

Eneo hili liko kaskazini-magharibi mwa Pakistan na liliunganishwa na jimbo la Khyber Pakhtunkhwa pamoja na maeneo mengine ya kikabila yapata miaka 5 iliyopita. Kwa hiyo, matarajio ya Mashia yalikuwa kwamba kwa uunganishaji huu, usalama wa eneo la Kurram ungeimarishwa na hivyo kuzuia kuendelea kwa jinai za vibaraka wenye mafungamano na Wazayuni huko Parachinar.

Lakini kiutendaji, serikali ya jimbo la Khyber Pakhtunkhwa, ambayo kwa kawaida iko mikononi mwa chama cha Imran Khan cha Tehreek-e-Insaf, haichukui hatua zozote za dhati kudhamini usalama wa Mashia wa Parachinar. Kwa muktadha huo, wawakilishi wa Bunge la Pakistan walipendekeza kwamba, kufuatia kushindwa kwa jeshi kusimamia  usalama katika mji wa Parachinar, kuanzishwe kikosi cha wananchi kinachojumuisha vijana wa Kishia na Kisunni ili kusimamia usalama wa eneo hilo.

Hamid Hussein mwakilishi wa Parachinar katika Bunge la Pakistan anaamini kuwa, wanaolengwa na magaidi katika eneo hilo sio Mashia pekee, kwani miezi michache iliyopita, msafara wa Masuni ulilengwa pia na uhalifu wa kigaidi katika sehemu hiyo hiyo, ambapo zaidi ya Watu 30 ambao ni Waislamu wa madhehebu ya Kisunni waliuawa. Kwa hiyo, tatizo si kadhia ya Shia na Sunni kwa sababu wafuasi wa madhehebu hayo mawili wamekuwa wakiishi pamoja kwa miaka mingi bila matatizo yoyote.

Kwa hivyo, serikali za majimbo na shirikisho za Pakistan zina jukumu zito la kukabiliana na magaidi.

Wakati serikali ya jimbo la Khyber Pakhtunkhwa inakabiliwa na kuenea kwa ugaidi katika eneo lake la usalama na haichukui hatua zozote za kuudhibiti, swali muhimu ni je, ni nini madhumuni ya maandamano makubwa yaliyofanyika kuelekea Islamabad? Hii ni katika hali ambayo, Pakistan inahitaji kuimarisha umoja wake wa kitaifa ili kukabiliana na changamoto zake muhimu, hasa usalama na harakati za kigaidi.