Umoja wa Mataifa watoa wito wa kuruhusiwa misaada ya kibinadamu Gaza
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali mbaya ya Gaza na kutoa wito wa kufikishwa mara moja kwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo, akisisitiza kwamba watu wa Gaza wanakabiliwa na njaa na kwamba ulimwengu unatazama hali hii.
Wito huo unatolewa wakati ambapo mgogoro wa kibinadamu huko Gaza umeongezeka kwa kasi na hitajio la misaada ya kibinadamu limefikia kilele chake. Msimamo wa Guterres unaweza kuweka shinikizo zaidi kwa Israel na jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka katika suala hili.
Katika radiamali yake kwa vikwazo vikali vya Israel vya kuingia misaada ya kibinadamu Gaza, Guterres ametangaza kuwa ni malori 50 tu kati ya 400 yaliyobeba misaada ya kibinadamu ndiyo yaliyoruhusiwa kuingia katika Ukanda huo. Kauli hizi zinakuja wakati Umoja wa Mataifa, kama chombo kinachohusika na misaada ya kibinadamu, ukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya watu wa Gaza.
Haya yanajiri huku wataalamu wa usalama wa chakula wakionya kuwa, Gaza inakabiliwa na baa la njaa iwapo mzingiro huo hautaondolewa, huku mashirika ya misaada yakiripoti kuwa yalimaliza akiba ya chakula wiki chache zilizopita. Takriban wakazi wote milioni 2.3 wa Gaza wanategemea chakula cha msaada.
Haya yanajiri huku utawala ghasibu wa Israel ukiendelea kufanya mauaji ya halaiki katika Ukanda wa Gaza. Zaidi ya Wapalestina 50 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya punde zaidi ya anga ya Israel kwenye jengo la makazi, kaskazini mwa Gaza.
Wizara ya Afya ya Gaza imesema watoto na wazee 29 waliofariki dunia katika siku za hivi karibuni Gaza wamewekwa katika orodha ya "vifo vinavyotokana na njaa", na maelfu zaidi wako hatarini kufa njaa.