Lavrov: Russia ni mshirika wa kuaminika kwa Afrika katika kuimarisha mamlaka
(last modified Tue, 27 May 2025 11:52:05 GMT )
May 27, 2025 11:52 UTC
  • Lavrov: Russia ni mshirika wa kuaminika kwa Afrika katika kuimarisha mamlaka

Sergey Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia amesema Moscow imebaki kuwa mshirika wa kweli na wa kuaminika kwa mataifa ya Afrika kwa kusaidia juhudi za kuimarisha mamlaka zao, ambazo zinatishiwa na aina za kisasa za ukoloni.

Lavrov alitoa kauli hiyo siku ya Jumatatu wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika yaliyoandaliwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia mjini Moscow, akihutubia mabalozi na maafisa wa Afrika.

Ameashiria msaada wa muda mrefu wa Russia kwa mataifa ya Afrika, ulioanza enzi za Umoja wa Kisovyeti (USSR) ambapo Moscow iliunga mkono harakati za ukombozi wa kitaifa na kusaidia katika kuangusha mifumo ya kikoloni.

Amesema:“Leo hii, Russia inaendelea kushiriki katika kuimarisha nafasi ya Afrika kama kitovu cha kipekee chenye ushawishi katika maendeleo ya dunia... Tutaendelea kusaidia mataifa ya Afrika katika kuimarisha uwezo wao wa kujilinda, kupambana na ugaidi, na kuhakikisha usalama wa chakula na nishati.”

Lavrov amesifu kaulimbiu ya Umoja wa Afrika kwa mwaka 2025 kama ishara ya juhudi za dunia kushughulikia dhuluma za kihistoria, na kukaribisha azimio la Umoja wa Mataifa linalotaka kuwe na siku maalum ya kimataifa ya kukabiliana na ukoloni. Amehimiza mashirikiano zaidi kuelekea ulimwengu wa haki wenye mihimili kadhaa ya kiutawala (multipolar world) na akasisitiza tena uungaji mkono wa Russia kwa nafasi ya Afrika katika uongozi wa dunia, ikiwemo uwakilishi wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Moscow imetangaza kuwa kukuza mahusiano na mataifa ya Afrika ni miongoni mwa vipaumbele vyake vikuu vya sera za nje, na kuongeza uwepo wake barani humo, ambapo mataifa kadhaa yakiwemo Afrika Kusini, Niger na Burkina Faso yanaiangalia kama mshirika wa kuaminika.

Lavrov amesisitiza tena dhamira ya Russia ya kuendeleza ushirikiano na mataifa ya Afrika kupitia majukwaa kama vile Kilele cha Russia na Afrika, na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa. Ametangaza kuwa mkutano wa mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya Russia na Afrika utafanyika katika nchi moja ya Afrika baadaye mwaka huu, na kuwa utaandaa mazingira ya mkutano wa tatu wa kilele mwaka 2026.