Spika wa Bunge la Mashariki Libya atoa mwito wa umoja wa kitaifa
Spika wa Bunge lenye makao yake mashariki mwa Libya, Aguila Saleh ametoa mwito wa kuundwa serikali mpya ya umoja wa kitaifa ili kusimamia uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu, na hivyo kuzidisha mzozo kati yake na serikali yenye makao yake makuu mjini Tripoli hasa kwa vile Aquila Saleh amemtaka Waziri Mkuu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ajiuzulu.
Akizungumza wakati wa kikao cha bunge mjini Benghazi, Saleh amewataka wabunge kuharakisha juhudi za kuunganisha taasisi za serikali.
Libya imegawanyika tangu mwaka 2014 kati ya tawala hasimu za mashariki na magharibi na hitilafu hizo hazijatatuliwa hadi hivi sasa licha ya kuweko juhudi za kuleta maridhiano zinazoungwa mkono mara kwa mara kimataifa.
Aquila Saleh amesema: "Suluhu ya mgogoro wa Libya ipo katika kufanya uchaguzi, lakini hii inahitaji kuwa na serikali yenye umoja inayokubaliwa na wote."
Aidha ameonya kwamba kucheleweshwa zaidi uchaguzi kunaweza kusababisha machafuko na hatati kwa umoja wa ardhi ya Libya, na ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa na wahusika wa ndani, ikiwa ni pamoja na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya (UNSMIL), kuunga mkono mchakato huo.
Saleh ametangaza kwamba Baraza la Wawakilishi lenye makao yake makuu mashariki mwa Libya litakutana hivi karibuni ili kumchagua waziri mkuu mpya, na amewaalika mabalozi wa nchi za nje, wawakilishi wa UNSMIL, na mashirika ya kiraia ya Libya kuhudhuria ili kuangalia kwa karibu mchakato huo.
Pendekezo hilo limeleta upinzani mkali kutoka kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa yenye makao yake makuu mjini Tripoli (GNU), inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdul Hamid Dbeibah.
Kufuatia mapigano ya hivi karibuni kati ya makundi hasimu yenye silaha mjini Tripoli, Saleh alitangaza kwamba Dbeibah anapaswa kuachia ngazi "kwa hiari au kwa nguvu."