Mwandishi maarufu wa Kenya , Ngũgĩ wa Thiong’o, afariki dunia
(last modified Thu, 29 May 2025 09:55:10 GMT )
May 29, 2025 09:55 UTC
  • Mwandishi maarufu wa Kenya , Ngũgĩ wa Thiong’o, afariki dunia

Ngũgĩ wa Thiong’o, gwiji wa fasihi ya Kiafrika na sauti isiyochoka ya ukombozi wa kiakili barani, ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 87, familia yake imethibitisha.

"Ni kwa moyo mzito tunapowaarifu kuhusu kifo cha baba yetu mpendwa, Ngũgĩ wa Thiong’o," aliandika binti yake, Wanjiku wa Ngũgĩ, kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa familia, Ngũgĩ alifariki siku ya Jumatano huko Atlanta, Marekani. Wanjiku amesema taarifa zaidi kuhusu kifo hicho zitatolewa hivi karibuni.

Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o alizaliwa mwaka 1938 nchini Kenya na atakumbukwa kama mmoja wa waandishi wa fasihi waliotengeneza njia mpya baada ya ukoloni. Maisha yake ya awali yaliathiriwa sana na vita vya Mau Mau, harakati za ukombozi zilizotikisa Kenya chini ya utawala wa Waingereza katika miaka ya 1950.

Ngũgĩ hakusita kukosoa ukandamizaji wa kikoloni pamoja na udhalimu wa mifumo ya baada ya uhuru. Aliandika kwa ujasiri kuhusu lugha, tamaduni, historia na utambulisho,  akiangazia mkanganyiko wa mwafrika aliyeachwa kusimama baina ya mila na mwelekeo wa Kimagharibi.

Katika miaka ya 1970, Ngũgĩ alichukua hatua ya kihistoria na yenye utata kwa kuacha kuandika kwa Kiingereza na badala yake akaandika kwa lugha za Kikuyu na Kiswahili, uamuzi uliovuta hisia kali na mijadala mikubwa.

Aliiandika moja ya kazi zake maarufu zaidi, 'Kuondoa Ukoloni wa Kifikra ' Decolonising the Mind  (1986), akiwa ughaibuni. Katika kazi hiyo, Ngũgĩ alitetea kwamba "haiwezekani kujikomboa kiakili kwa kutumia lugha ya mkoloni."

Rais wa Kenya, Dkt. William Ruto, ameongoza Wakenya na Waafrika kwa ujumla kuomboleza kifo cha Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o. Kupitia ujumbe aliouandika katika ukurasa wake wa X, Rais Ruto amemtaja Ngũgĩ kuwa mtu shujaa na mwenye maono.

"Aliacha alama isiyofutika katika namna tunavyotafakari uhuru wetu, haki ya kijamii na matumizi  ya madaraka ya kisiasa na kiuchumi," amesema Rais Ruto.