Siku 600 za mauaji ya kimbari Gaza, Israel yaendeleza jinai
(last modified Thu, 29 May 2025 10:02:51 GMT )
May 29, 2025 10:02 UTC
  • Siku 600 za mauaji ya kimbari Gaza, Israel yaendeleza jinai

Tangu kuanza kwa mashambulizi makubwa ya utawala wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mnamo Oktoba 2023, hadi Jumatano tarehe 28 Mei 2025, ikiwa ni siku ya 600 ya vita, maisha ya kiraia katika eneo hilo yameporomoka kabisa chini ya mashambulizi yasiyokoma ya Wazayuni.

Kwa mujibu wa ripoti huru na mashirika ya kimataifa, zaidi ya Wapalestina 54,000 wameuawa katika mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na utawala katili wa Israel, huku wengine 123,000 wakijeruhiwa, wengi wao wakiwa wanawake, watoto na wazee. Hii ni hali ya janga la kibinadamu lisilo na mfano wake, likiendelea mbele ya macho ya dunia nzima.

Utawala wa Israel unaendelea kupata msaada wa kijeshi, kiuchumi na kisiasa kutoka Marekani, huku ukiendeleza mauaji ya kimbari, ukandamizaji na uharibifu wa makusudi wa miundombinu ya raia.

Wataalamu wa misaada ya kibinadamu wanasema hali ya Gaza sasa ni mbaya zaidi kuliko ilivyowahi kushuhudiwa katika historia ya kisasa. Asilimia zaidi ya 80 ya ardhi ya kilimo imeharibiwa, na Umoja wa Mataifa kupitia Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) unakadiria kuwa asilimia 95 ya ardhi hiyo sasa haiwezi kutumika kwa uzalishaji wa chakula, hali inayoongeza hatari ya baa la njaa.

Huduma za afya zimeporomoka. Kati ya vituo 22 vya afya vya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbiri wa Palestina, UNRWA, ni vituo sita pekee vinavyofanya kazi. Dawa zimekwisha, vifaa vya upasuaji havipo na wagonjwa wanakufa kutokana na magonjwa yanayoweza kutibiwa kwa urahisi iwapo huduma zingepatikana.

Kufikia Januari 2024, takribani asilimia 62 ya majengo yote Gaza yalikuwa yameharibiwa au kusambaratishwa, kiwango cha uharibifu kinachozidi hata maeneo mengi ya vita yaliyoshuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni.

Katika hali ya kusikitisha na inayozidi kuwa hatari kwa maisha ya binadamu, uwezo wa uzalishaji wa maji katika Ukanda wa Gaza umepungua kwa asilimia 95.

Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa tani milioni 42 za vifusi zimesalia Gaza. Kwa kasi ya sasa, kusafisha na kuijenga Gaza upya kunaweza kuchukua hadi miaka 80 na kugharimu zaidi ya dola bilioni 80 za Kimarekani.

Kinachoshuhudiwa Gaza si vita ya kawaida; ni uharibifu wa eneo zima na wa makusudi. Majumba, shule na hospitali, zimefutwa  kabisa kwenye ramani. Utawala wa Israel sasa uko chini ya uchunguzi mkali wa sheria za kimataifa. Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) imetoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa Vita, Yoav Gallant. Wakati huo huo, Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) inasikiliza mashitaka ya mauaji ya kimbari dhidi ya utawala huo.

Wakati vita vya mauaji ya kimbari Gaza vikiwa vimeingia siku yake ya 600, watu wa Gaza hawana pa kukimbilia. Hakuna usalama. Hakuna msaada mkubwa wa kimataifa. Kile kilichobakia ni vifusi, njaa na huzuni, huku dunia ikiendelea kujadiliana na kutazama tu kwa mbali hali hiyo ya kusikitisha.