Rais Pezeshkian: Iran iko tayari kushirikiana kuthibitisha malengo ya amani ya nyuklia
(last modified Thu, 29 May 2025 10:45:17 GMT )
May 29, 2025 10:45 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran iko tayari kushirikiana kuthibitisha malengo ya amani ya nyuklia

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran, amesema kuwa nchi yake iko tayari kushirikiana kikamilifu kwa njia yoyote ile ili kudhihirisha kuwa shughuli zake za nyuklia ni za amani, lakini haitakubali kwa vyovyote vile kuacha haki yake ya kimsingi ya kurutubisha madini ya urani.

Akizungumza katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Oman wakati wa ziara yake ya karibuni katika nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi siku ya Jumatano, Rais Pezeshkian amesema: "Iwapo kuna haja ya kuhakikisha kuwa hatufuatilii silaha za nyuklia, tuko tayari kushirikiana kwa njia yoyote ile kuhakikisha ulimwengu na kanda hii wanajua wazi kuwa hatufanyi hivyo, hatujawahi kufanya na hatutafanya kabisa."

Ameongeza kuwa amri ya kidini (fatwa) iliyotolewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, imepiga marufuku wazi wazi juhudi zozote za Iran kutengeneza silaha za nyuklia.

Licha ya hayo, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran itaendelea na urutubishaji wa madini ya urani kwa madhumuni ya amani kama vile matibabu na uchunguzi wa kitabibu, maendeleo ya kilimo pamoja na uboreshaji wa viwanda.

Amesema shughuli hizo zinafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa, na Iran haitakubali kushinikizwa kusitisha shughuli zake za urutubishaji urani.

Kuhusu masharti muhimu ya kufikiwa kwa makubaliano yoyote na Marekani, Rais Pezeshkian amesema:

"Masharti ni yale yale yanayowekwa na sheria za kimataifa, kila nchi ina haki ya kufanya utafiti wa kisayansi katika urutubishaji wa urani na matumizi ya nishati ya nyuklia kwa njia za amani."

Aidha, amipongeza Oman kwa juhudi zake za upatanishi ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa Iran kufanikisha malengo yake katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Marekani yaliyoanza mwezi Aprili.

Kuhusu uhusiano wa Iran na Oman, Rais Pezeshkian amesema kuwa ushirikiano wa kisiasa kati ya mataifa haya uko katika kiwango cha juu zaidi.

Aidha amesema mataifa haya mawili yana mtazamo unaofanana kuhusu masuala ya kikanda, ikiwemo msimamo wao wa pamoja kuhusiana na suala la Palestina.