Araghchi: Iran haitaruhusu kuvurugwa kwa uhusiano na Saudi Arabia
Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, amesisitiza dhamira ya Iran ya kudumisha uhusiano wa "kidugu" na Saudi Arabia, akisema kuwa Tehran haitakubali yeyote kuvuruga mahusiano hayo muhimu kwa ulimwengu wa Kiislamu.
Shirika rasmi la Habari la Iran IRNA, leo Alhamisi limemnukulu Aragchi akisema: "Tuko makini kabisa kuhusu uhusiano wetu na Saudi Arabia. Sera yetu ya ujirani mwema, ambayo si mpya, ni muhimu sana. Saudi Arabia inashikilia nafasi ya kipekee katika sera hii, na tutaendeleza uhusiano wetu wa kindugu na hatutaruhusu kuvurugwa uhusiano huu."
Akizungumzia kukamatwa kwa mmoja wa Mahujaji wa Iran na polisi wa Saudi Arabia katika mji wa Madina, Waziri huyo ameongeza kuwa Tehran iko katika mawasiliano ya karibu na maafisa wa Iran walioko Saudi Arabia ili kuhakikisha kuwa hakuna usumbufu wowote katika kupeleka Mahujaji kwa ajili ya ibada ya Hajj na kushughulikia changamoto zinazojitokeza.
Kupitia chapisho lake kwenye akaunti ya X siku ya Jumanne, Araghchi alisema Iran inalaani vikali jaribio lolote la kuhujumu umoja wa Kiislamu, hasa katika mazingira ya kiroho ya ibada ya Hija.
Aidha ameandika kuwa: "Tumeazimia kutoruhusu yeyote kuhujumu uhusiano wetu wa kindugu na majirani zetu, ikiwemo njia ya maendeleo ya Iran na Saudi Arabia."
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Saudi Arabia, Abdulaziz bin Saud bin Naif bin Abdulaziz Al Saud, alisema siku ya Jumatano kuwa uhusiano mzuri na chanya kati ya Iran na Saudi Arabia utakuwa na manufaa kwa ulimwengu wa Kiislamu na kanda nzima.
Alitoa kauli hiyo katika kikao chake na Mkuu wa Taasisi ya Hija na Umra ya Iran, Alireza Bayat, kilichofanyika mjini Jeddah ambapo walijadili masuala mbalimbali ya pande zote mbili.
Waziri huyo alisema kuwa Saudi Arabia itaendelea kushirikiana kwa karibu na Iran katika kushughulikia mahitaji ya ushirikiano baina ya taasisi mbalimbali ili kutatua changamoto zinazowakabili Mahujaji wa Iran.
Aliongeza kwa kupongeza uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizi mbili kama matokeo ya nia njema za pande zote.
Waziri huyo alisisitiza kuwa Saudi Arabia ina nia ya dhati ya kutekeleza kanuni na taratibu zinazolenga kulinda usalama na amani ya Mahujaji wote wanaofika kutoka pande mbalimbali za ulimwengu kwa ajili ya kutekeleza ibada ya Hajj.
Pia alitoa shukrani kwa maafisa na Mahujaji wa Iran kwa ushirikiano wao mzuri na serikali ya Saudi Arabia.
Kwa upande wake, afisa huyo wa Iran ameipongeza serikali ya Saudi Arabia kwa jitihada zake za kuwezesha utekelezaji wa ibada ya Hajj kwa urahisi na usalama.
Amesema Iran iko tayari kuendeleza mazungumzo zaidi na Saudi Arabia ili kusuluhisha masuala yoyote yanayojitokeza katika muktadha huo.