Onyo la Trump kwa Netanyahu baada ya kutishia kuishambulia Iran
Rais wa Marekani, Donald Trump ameripotiwa kuvutana na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu katika mazungumzo yao ya simu, baada ya nduli huyo wa vita wa utawala wa Kizayuni kutishia kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, na hivyo kuhatarisha mazungumzo ya kidiplomasia yanayoendelea kati ya Tehran na Washington.
Katika mazungumzo hayo, Netanyahu alimwambia Trump kwamba "sasa ni wakati mwafaka wa kuchukua hatua za kijeshi," akiashiria kuwa diplomasia haina tija.
Trump, hata hivyo, hakukubaliana na msimamo huo wa Netanyahu, akisema hii ni "fursa nzuri ya mazungumzo," hatua inayoashiria mvutano wa muda mrefu kati ya viongozi hao wawili kuhusu jinsi ya kukabiliana na Iran.
Rais wa Marekani amesisitiza kuwa, mashambulizi ya Israel dhidi ya Iran 'hayafai kufanya hivi sasa kwa sababu tuko karibu sana kufikia suluhu.'
Washington na Tel Aviv kwa muda sasa zimeendelea kugawanyika kuhusu jinsi ya kukabiliana na makubaliano ya nyuklia ya Iran. Wakati timu ya Trump inafuatilia mfumo wa kupunguza mvutano, Netanyahu anashinikiza kutumiwa njia ya mabavu zaidi na ya kijeshi.
Mgawanyiko huo unaonyesha tofauti kubwa za kijiografia kati ya washirika hao wawili huku eneo la Asia Magharibi likiwa katika ncha ya kutumbukia kwenye mzozo mwingine unaonukia.
Hii ni katika hali ambayo, utafiti mpya uliofanywa nchini Marekani umeonyesha kuwa, asilimia kubwa ya Wamarekani wanataka kufikiwa mkataba mpya wa amani na Iran, huku kukiwa na upinzani mkubwa dhidi ya hatua yoyote ya kijeshi.