Balozi wa Israel atimuliwa na waungaji mkono Palestina, Senegal
Balozi wa Israel nchini Senegal, Yuval Waks, alilazimika kuondoka katika Chuo Kikuu cha Dakar baada ya wanafunzi kupinga uwepo wake na kupiga nara za kuunga mkono Palestina chuoni hapa.
Waks alikuwa amealikwa kuhutubia mkutano kuhusu mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Cheikh Anta Diop (UCAD), taasisi kubwa na maarufu zaidi ya elimu ya juu nchini humo.
Lakini alipofika, makumi ya wanafunzi walikusanyika nje ya ukumbi, wakiimba "Palestina Huru," "Gaza Huru" na "Israel ni mhalifu wa vita."
Video zilizosambaa mitandaoni zinaonyesha wanafunzi wakipeperusha bendera za Palestina na kumzomea mjumbe huyo mpya, sambamba na kumzuia kutoa hotuba yake.
Waks aliondolewa haraka na maafisa usalama chuoni bila kuhutubia hadhira. Waandamanaji waliendelea kumfuata huku wakipiga kelele na kupeperusha bendera alipokuwa akiondoka.
Waks, ambaye pia anahudumu kama balozi asiye mkaaji wa Israel nchini Gambia, Guinea, Guinea-Bissau, Cape Verde na Chad, aliwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye mnamo Mei 8.
Maandamano makubwa yamekuwa yakifanyika katika mji mkuu wa Senegal, Dakar kupinga jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza.
Aidha wasanii wa Senegal wamechora jumbe za kuunga mkono Palestina na Lebanon kwenye kuta za Dakar huku wakibainisha kuchukizwa kwao na jinai za Israel.