Jeshi la Marekani latafakari kuondoka Afrika
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani barani Afrika (AFRICOM) ametangaza mpango wa kutathmini upya uwepo wa jeshi hilo katika bara la Afrika, huku mataifa mengi yakianza kupima upya ushirikiano wao wa kiulinzi na nchi za Magharibi na kuelekeza ushirikiano wao kwa nchi zingine zisizo za kibeberu.
Hatua hii inakuja miezi michache baada ya Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) kulazimika kuondoa majeshi yake kutoka nchi kadhaa za eneo la Sahel barani Afrika.
Kamanda wa AFRICOM, Jenerali Michael Langley, amewaambia waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, kwamba tayari ameshafanya mazungumzo na mawaziri wa ulinzi pamoja na baadhi ya wakuu wa nchi barani Afrika kuhusu suala hilo. Langley yuko nchini Kenya kushiriki kongamano la makamanda wa majeshi ya Afrika liloloanza jana.
Amesema: “Nimezungumza na mawaziri wa ulinzi kadhaa na marais wachache na kuwaeleza kuwa tunafanya tathmini."
Hatua hii inajiri sambamba na taarifa zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Marekani zikidai kuwa serikali ya Rais Donald Trump inatafakari kuunganisha AFRICOM na Kamandi ya Kijeshi ya Ulaya ya Marekani (EUCOM) yenye makao yake Stuttgart, Ujerumani, kwa lengo la kuongeza ufanisi wa kiutendaji.
AFRICOM ilianzishwa mwaka 2008, ambapo lengo la kidhahiri lilotajwa lilikuwa ni kuratibu juhudi za kijeshi za Marekani barani Afrika na kujibu changamoto zinazoongezeka za kiusalama. Hata hivyo, tangu kuanzisha AFRICOM si tu kuwa ugaidi haukupungua, bali umekuwa ukiongezeka barani Afrika na hivyo kutilia shaka lengo hasa la jeshi la Marekani barani humo.
Marekani awali ilisisitiza nia yake ya kuendeleza uwepo wa kijeshi katika ukanda huu licha ya kushinikizwa kuondoa wanajeshi wake kutoka maeneo muhimu, hasa mataifa ya Sahel kama Niger na Chad.
Mwezi Septemba mwaka jana, Pentagon ilikamilisha kuondoa vifaa na takriban wanajeshi 1,000 kutoka kituo chake cha kijeshi chenye thamani ya dola milioni 100 kilichoko Niger, kufuatia amri kutoka kwa serikali ya kijeshi ya nchi hiyo ya Afrika Magharibi, iliyosema kuwa kikosi hicho cha Marekani kilishindwa kudhibiti mashambulizi ya makundi ya kigaidi huko Sahel.
Wizara ya Ulinzi ya Marekani pia iliondoa takriban wafanyakazi 70 kutoka kituo cha anga karibu na mji mkuu wa Chad, N’Djamena baada ya kutakiwa kufanya hivyo na serikali ya Chad.
Ufaransa pia imelazimika kuondoa majeshi yake na kusitisha ushirikiano wa kijeshi na Burkina Faso, Niger na Mali, huku tawala mpya katika mataifa hayo zikigeukia ushirikiano mbadala, hasa kuimarisha mahusiano ya kijeshi na Russia.