Mgogoro wa kibinadamu Sudan unazidi kuongezeka, mapigano yanaendelea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i126926-mgogoro_wa_kibinadamu_sudan_unazidi_kuongezeka_mapigano_yanaendelea
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan unazidi kuongezeka huku mapigano yakiendelea, watu wanazidi kuhama makazi yao na udharura wa kuchukuliwa hatua za kiafya umezidi kuwa mkubwa.
(last modified 2025-05-28T07:16:36+00:00 )
May 28, 2025 07:16 UTC
  • Mgogoro wa kibinadamu Sudan unazidi kuongezeka, mapigano yanaendelea

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema kuwa mgogoro wa kibinadamu nchini Sudan unazidi kuongezeka huku mapigano yakiendelea, watu wanazidi kuhama makazi yao na udharura wa kuchukuliwa hatua za kiafya umezidi kuwa mkubwa.

Sehemu moja ya taarifa ya OCHA imesema: Katika jimbo la Darfur Kaskazini, mashambulizi ya mizinga na risasi yanaendelea kuathiri maeneo ya makazi ya raia katika mji wa El Fasher na kambi ya wakimbizi ya  Abu Shouk yenye wakimbizi wengi wa ndani. Mauaji ya kila siku ya raia yanaripotiwa na siku za hivi karibuni zimeshuhudia kuongezeka mashambulizi ya mabomu nyakati za usiku.

"Washirika wa misaada ya kibinadamu wameripoti kuwa, upatikanaji wa elimu unaendelea kuwa na vikwazo vikali huko Darfur Kaskazini. Tangu mzozo huo uanze Aprili 2023, robo milioni ya watoto wamepoteza fursa ya kujifunza nchini Sudan," taarifa hiyo imesema.

Huko katika jimbo la Kordofan Kusini, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji liliripoti wiki iliyopita kwamba takriban watu 2,800, hasa wanawake na watoto, wamekimbia mapigano mapya katika mji wa Dibebad. Hali katika makao makuu ya jimbo la Kadugli pia imezorota sana katika wiki za hivi karibuni, huku makombora makali yakizidi kupiga mji huo na kusababisha ufikishaji wa misaada ya kibinadamu kukwama kikamilifu.

Serikali za kieneo zimeripoti kwamba takriban watu 6,000 waliokimbia makazi yao katika majimbo ya Darfur Kaskazini, Khartoum na Kordofan Magharibi kutokana na ukosefu wa usalama walifika katika eneo la Ad Dabbah kati ya Mei 12 na 22 na wanahitaji misaada mingi ya kibinadamu. 

Wakati huo huo, mripuko wa ugonjwa kipindupindu katika jimbo la Khartoum unazidi kuwa mbaya kwa kasi ya kutisha. Mashirika ya misaada ya kibinadamu katika jimbo hilo yameripoti kuweko ongezeko la asilimia 80 la kesi za kipindupindu kwenye kipindi cha wiki mbili zilizopita huko Khartoum pekee.