Je, kwa nini Israel haiwezi kuishinda Hamas?
(last modified Tue, 27 May 2025 02:56:15 GMT )
May 27, 2025 02:56 UTC
  • Je, kwa nini Israel haiwezi kuishinda Hamas?

Madai ya maafisa wa baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu Wazir Mkuu wa utawala ghasibu wa Israel kuhusu kushindwa Hamas yameibua utata katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, ambapo wachambuzi wengi na maafisa wa utawala huo wa kizayuni wanayachukuliwa kuwa ni uongo na uzushi mtupu.

Gazeti la Kizayuni la Yedioth Ahronoth, likinukuu vyanzo vya habari, limeripoti mabishano makali kati ya Amit Halevi, mwanachama wa Knesset kutoka chama cha Likud na Yisrael Katz, Waziri wa Vita wa Israel wakati wa kikao katika bunge hilo la Kizayuni. Gazeti hilo limeripoti kuwa, Halevi alimwambia waziri huyo wa vita kuwa haelewi chochote na kwamba hakuna mpango wowote utakaoishinda Hamas. Halevi amesema: "Tumekuwa vitani kwa muda wa miezi 20 na bado tunaendelea kutekeleza mipango iliyofeli kijeshi. Israel imeshindwa kuiangamiza Hamas. Hatuna uwezo wa kuishinda Hamas."

Awali, Avigdor Lieberman, kiongozi wa chama cha Yisrael Beitenu, pia alisema kwamba mtu ambaye ameshindwa kuiangamiza Hamas katika kipindi cha miezi 20 iliyopita hatafanikiwa kufanya hivyo hata akipewa miaka mingine 17. Hali halisi ya nyanjani, ikiwa ni pamoja na makubaliano ya hivi karibuni ya Marekani na Hamas, pia yanaonyesha kwamba madai ya Israel kuhusu kushinda na kuiangamiza Hamas ni uongo mtupu unaokusudia kuhadaa fikra za waliowengi ulimwenguni, na kwamba Hamas bado iko hai na inachukuliwa kuwa moja ya makundi muhimu ya kisiasa nchini Palestina, hususan katika Ukanda wa Gaza. Swali ni kwamba je, kwa nini Israel inayodaiwa kuwa nguvu kubwa ya kijeshi duniani haijafanikiwa kuishinda Hamas, na ni sababu gani zimeifanya Hamas iendelee kusimama imara?

Kuna sababu kadhaa kuhusiana na suala hili, ikiwa ni pamoja na:

1- Hamas ni itikadi inayoungwa mkono na watu wengi.

Ukweli wa mambo ni kwamba Hamas ni zaidi ya harakati na chama. Guido Steinberg, mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati katika Taasisi ya Kijerumani ya Masuala ya Kimataifa na Usalama anasema: "Hamas ni harakati ya kijamii yenye uungwaji mkono mkubwa katika Ukanda wa Gaza na hata Ukingo wa Magharibi." Kwa hiyo, Hamas haitaangamizwa kwa kuuliwa makamanda wake na ina uwezo wa kujijenga upya.

Wapiganaji wa Hamas kwenye maji

2- Fikra ya Hamas kuhusu Palestina inaungwa mkono na watu wengi.

Sababu nyingine muhimu ya siri ya kuendelea kuwepo kwa muda mrefu harakati hii ya muqawama wa Palestina ni kwamba fikra ya Hamas ya kuikomboa Palestina na kuunda taifa huru la Palestina ni fikra iliyokita mizizi na ya kihistoria miongoni mwa wananchi wa Palestina na ina uungaji mkono mkubwa katika taifa hilo. Licha ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni, wananchi wa Palestina wanaendelea kujivunia utambulisho wao wa Palestina na hawako tayari kuachana na kadhia ya ukombozi wa Palestina. Hamas pia imechagua njia ya mapambano kwa ajili ya kufikia ukombozi wa Palestina. Kwa hivyo, Hamas imesalia na itasalia kuwa nguvu ya kisiasa yenye ushawishi mkubwa miongoni mwa Wapalestina, ambapo utawala wa Kizayuni hauwezi kuishinda wala kuitokomeza kabisa.

3- Mbinu ya kupigana Hamas imepelekea Israeli ishindwe kukabiliana nayo.

Mbinu ya Hamas kupigana kwenye medani ya vita ni kwamba haitegemei watu binafsi; bali hata kwa kukosekana makamanda, vikosi vya Hamas vinaweza kutekeleza mbinu zao za kijeshi. Vikosi vya Hamas bado vinaweza kuvisababishia hasara kubwa vikosi vya Israeli kwenye vita vya nchi kavu na vya mijini. Mbinu hii ya vita imeiwezesha Hamas kuzuia uwepo wa kudumu wa Israel katika Ukanda wa Gaza, na hivyo kuifelisha kijeshi na kuifanya isifikie malengo yake ya vita katika ukanda huo.

Kutokana na sababu zilizotajwa za kisiasa, kiitikadi na kijeshi, viongozi na wachambuzi wa Kizayuni wanaendelea kuamini kwamba matamshi yaliyotolewa na Netanyahu na baraza lake la mawaziri kuhusu kushindwa Hamas ni madai matupu yasiyo na mshiko na ambayo yanakusudia tu kuhadaa maoni ya umma kieno na kimataifa.