Iran yagundua na kusambaratisha karakana ya Mossad ya kuunda droni karibu na Tehran
Maafisa wa usalama wa Iran wamevamia makazi ya ghorofa tatu nje kidogo ya Tehran, ambapo wamegundia kituo cha siri kinachoendeshwa na shirika la kijasusi la Israel, Mossad, kwa ajili ya kuunganisha droni na vilipuzi.
Jumapili, polisi walitoa picha zilizoonyesha sehemu za droni, yakiwemo mabawa na sehemu za injini, pamoja na vifaa vya chuma vilivyotumika kwa utengenezaji.
Kwa mujibu wa maafisa husika, droni zilikuwa zikitengenezwa ndani ya nyumba hiyo, huku vifaa vya kutengenezea vipuri navyo vikikamatwa.
Ugunduzi huu unalingana na madai ya awali ya Israel yaliyoripotiwa na tovuti ya Axios, ambapo maafisa wa Mossad walikiri kusafirisha droni nchini Iran kwa kipindi cha miezi minane ili kulenga miundombinu ya makombora.
Gazeti la The Guardian limedokeza kwamba maajenti wa Mossad walikuwa wamejipenyeza karibu na maeneo ya vituo vya ulinzi wa anga ya Iran kwa ajili ya hujuma iliyoratibiwa kwa kutumia droni.
Ugunduzi wa karakana hiyo ni ushahidi wa wazi wa operesheni za Mossad ndani ya ardhi ya Iran, huku Israel ikiendeleza vita dhidi ya Iran na Ukanda wa Gaza.
Katika tukio lingine lililotokea Jumapili, klipu zilionesha msururu wa magari yakikimbizana kwa kasi katika barabara za Tehran.
Afisa wa usalama wa Iran alifukuza lori lililoshukiwa kubeba droni za hali ya juu za Israel.
Kwa kufyatua risasi mbili zilizolenga shabaha kwa usahihi wa hali ya juu, afisa huyo alifanikiwa kusimamisha gari hilo, na kunasa droni za kisasa zilizounganishwa kwa ajili ya kutekeleza ugaidi kwa niaba ya utawala wa Israel.
Wiki za hivi karibuni Iran imekamata idadi kubwa ya majasusi wa Mossad na madola mengine ajinabi.
Maafisa wa usalama wameahidi kudumisha umakini huku kukiwa na mivutano mikali ya kikanda, wakisisitiza azma ya Iran ya kukabiliana na vitisho kutoka Israel na washirika wake.
Maafisa wa usalama wa Iran wamesisitiza mara kwa mara kwamba watu wa Iran wako macho katika kukabiliana na jinai za utawala wa Israel, ambao umekuwa ukitekeleza njama dhidi ya Iran kwa miongo kadhaa tokea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.