Jeshi la Iran lawaonya walowezi Waisraeli: Ondokeni muokoe maisha yenu
Majeshi ya Iran yametoa onyo kali kwa walowezi Waisraeli walio katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa kimabavu (Israel) na kuwataka waondoke mara moja, huku Iran ikijiandaa kutekeleza mashambulizi makubwa yanayotarajiwa kuenea katika ardhi zote zinazokaliwa kwa mabavu.
Kupitia ujumbe uliorushwa hewani Jumapili, Kanali Reza Sayyad, Msemaji wa Kituo cha Mawasiliano cha Vikosi vya Majeshi ya Iran, amewaonya walowezi hao kuwa kubaki katika maeneo hayo kutahatarisha maisha yao pakubwa. Iran inajipanga 'kulipiza kisasi kikali' kufuatia uchokozi wa kijeshi wa hivi karibuni kutoka Israel.
'Ondokeni maeneo yanayokaliwa kwa mabavu. Kuondoka katika ardhi hii iliyoghusubiwa ndiyo njia pekee ya kulinda maisha yenu,' amesisitiza Kanali Sayyad katika taarifa hiyo ya video, huku akilaani 'utawala wa Kizayuni' kwa uchokozi wake wa jinai dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Sayyad amekemea utawala wa waziri mkuu Netanyahu akieleza kuwa 'umekata tamaa, umejaa ufisadi, na ni wa kihalifu,' akisema kuwa uchokozi wao wa hivi karibuni wa kijeshi 'utaibua maangamizi'. Ametoa onyo kuwa majibu ya Iran yatalenga maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu.
Ameendelea kueleza kuwa jeshi la Iran lina 'idadi kubwa ya taarifa za kijasusi' kuhusu maeneo nyeti katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel, huku akiwaonya walowezi kuepuka maeneo hayo na kubainisha kuwa hata maficho ya chini ya ardhi hayatadhamini usalama wao.
Amesema utawala wa Israel unawatumia walowezi kama ngao ya binadamu, akiongeza kuwa vitendo vya utawala huo, vinavyochochewa na maslahi ya kisiasa na binafsi, vinapeleka eneo la Asia Magharibu kutumbukia katika mgogoro mkubwa zaidi.
'Utawala wa Kizayuni ni wa kihalifu, hasa waziri mkuu wake mhalifu, ameanzisha uhalifu kwa ajili ya maslahi yake binafsi na ya familia yake, uhalifu ambao utaishia kwa kushindwa na majuto.'
Ameongeza kuwa kupuuza maonyo ya Iran kutawasababishia 'siku ngumu zaidi' wale watakaobaki katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.
Matamshi ya Sayyad yamefuatia wimbi jipya la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani yaliyozinduliwa na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) Jumapili mchana kama sehemu ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli III.
Mashambulizi hayo yamesababisha milipuko mikubwa katika maeneo ya Galilee ya Juu na ya Chini, Haifa, Afula na Nazareth.
Operesheni hii ni jibu la moja kwa moja kwa uchokozi wa Israei dhidi ya Iran ambao ulianza Ijumaa asubuhi, na ambao umepelekea kuuawa shahidi makamanda wakuu wa kijeshi, wanasayansi wa nyuklia na raia wa kawaida, wakiwemo wanawake na watoto.