Kiongozi Muadhamu: Hatua madhubuti zinahitajika kukomesha jinai za Ghaza
(last modified Tue, 27 May 2025 02:56:37 GMT )
May 27, 2025 02:56 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Hatua madhubuti zinahitajika kukomesha jinai za Ghaza

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitizia ulazima wa kuweko hatua za pamoja na zenye ufanisi baina ya Iran na Pakistan za kukomesha jinai za utawala wa Kizayuni huko Ghaza na ameashiria nafasi maalumu ya Pakistan katika ulimwengu wa Kiislamu.

Kiongozi Muadhamu alisema hayo jana jioni wakati Waziri Mkuu wa Pakistan, Shahbaz Sharif na ujumbe aliofuatana nao walipokwenda kumtembelea ofisini kwake hapa Tehran. 

Mwanzoni mwa mazungumzo hayo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameelezea kuridhishwa kwake na kumalizika vita kati ya Pakistan na India na kusema kuwa, ana matumaini ya kuona zinatatuliwa tofauti za nchi hizo mbili kwa njia ya amani.

Vile vile ameashiria misimamo mizuri na thabiti ya Pakistan katika miaka ya hivi karibuni kuhusu kadhia ya Palestina na kusema: "Wakati katika miaka ya hivi karibuni kumekuwa na vishawishi kwa nchi za Kiislamu kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni, lakini Pakistan haijawahi kuathiriwa na vishawishi hivyo."

Akikumbushia uwezo mkubwa wa Umma wa Kiislamu wa kuwa na kauli na heshima kubwa zaidi katika dunia ya leo, Ayatullah Khamenei amesema: Katika hali ambayo watu wanaochochea vita duniani wana malengo mengi ya kuzusha machafuko na vita, jambo pekee linaloweza kuuhakikishia usalama Umma wa Kiislamu ni umoja na mshikamano baina ya nchi za Kiislamu na kuendeleza uhusiano mzuri kati ya nchi hizo.

Ameitaja kadhia ya Palestina kuwa ni suala la kwanza la ulimwengu wa Kiislamu na huku akiashiria hali ya kusikitisha mno ya Ghaza amesema: Hali ya Ghaza imefikia mahali ambapo hata watu wa kawaida wa Ulaya na Marekani wanaandamana dhidi ya serikali zao, lakini katika mazingira hayo hayo, kwa bahati mbaya baadhi ya serikali za nchi za Waislamu zinasimama upande wa utawala wa Kizayuni.

Akisisitiza kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Pakistan zinaweza kuuletea manufaa makubwa Ulimwengu wa Kiislamu kwa kushirikiana na kulitatua suala la Palestina, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: "Tuna matumaini makubwa kuhusu mustakbali wa Ulimwengu wa Kiislamu, na matukio mengi yanathibitisha usahihi wa imani yetu hiyo."

Katika mazungumzoa hayo ambayo yamehudhuriwa pia na Rais Pezeshkian, Bwana Shahbaz Sharif amesema kuwa amefurahishwa sana na kukutana na Kiongozi wa Mapinduzi na amepongeza nafasi chanya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuzima mgogoro uliozuka kati ya Pakistan na India. Pia amesema: "Kwa bahati mbaya, jamii ya kimataifa haichukui hatua madhubuti za kukomesha maafa ya Ghaza."