Jeshi la Iran: Tutakabiliana na tishio lolote au uchokozi kwa irada kamili
(last modified Sat, 24 May 2025 13:01:24 GMT )
May 24, 2025 13:01 UTC
  • Jeshi la Iran: Tutakabiliana na tishio lolote au uchokozi kwa irada kamili

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetangaza kuwa, litajibu kwa nguvu zake zote tishio au uchokozi wowote na halitaruhusu ndoto za maadui kutimia.

Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa tangazo hilo kwa mnasaba wa kumbukumbu ya kukombolewa mji wa Khorramshahr.

Taarifa hiyo ilisema kuwa jeshi, pamoja na vikosi vingine vya jeshi, viko tayari kutetea umoja wa ardhi ya Iran, uhuru, na usalama wa kitaifa, na kwamba kamwe halitaruhusu maadui wanaojificha fursa ya kutafsiri ndoto zao za fujo kuwa ukweli.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa: "Tarehe tatu ya Khordad ni siku ya kumbukumbu ya kukombolewa mji wa Khorramshahr, ni alama ya uimara na muqawama, na ushindi wa damu dhidi ya upanga. Siku hii kuu ni kumbukumbu ya mashujaa wa Uislamu katika Operesheni Beit al-Maqdis na inadhihirisha ujumbe usioweza kufa wa hayati Imam Khomeini: Khorramshahr imekombolewa."

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, "Kukombolewa kwa Khorramshahr kuliashiria mabadiliko makubwa katika historia ya Kujihami Kutakatifu na kuthibitisha kwamba kwa imani, umoja, na kumtegemea Mwenyezi Mungu, ushindi dhidi ya jeshi lolote unawezekana. Kwa sababu hiyo, Amiri Jeshi Mkuu alisisitiza haja ya kuhifadhi na kulinda mafanikio haya makubwa."

Miaka 43 iliyopita katika siku kama ya leo, mji wa Khorramshahr wa Iran ulikombolewa na wapiganaji wa Kiislamu na ukaondoka katika uvamizi wa majeshi vamizi ya Iraq. Mji wa Khorramshahr uko katika mkoa wa Khozestan kusini magharibi mwa Iran. Mji huo ulikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya Iraq kwa muda wa karibu mwaka mmoja na miezi minane.