Watanzania wanashiriki uchaguzi wa serikali za mitaa
Baada ya kampeni zilizotawaliwa na patashika nyingi, Watanzania leo watafanya uamuzi wa kuwachagua viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji watakaohudumu kwa miaka mitano ijayo.
Zaidi ya vijiji na vitongoji 75,000 vitachagua wawakilishi wao katika zoezi la uchaguzi unaofanyika baada ya miezi kadhaa ya mivutano ya kisiasa na ripoti za kutoweka kwa baadhi ya wapinzani wa kisiasa. Uchaguzi wa leo unafanyika mwaka mmoja kabla ya uchaguzi wa rais.
Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wasimamizi wa uchaguzi na wanaohusika, kuhakikisha uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji unakuwa wa haki, uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau.
"Nawasihi wasimamizi wa uchaguzi na wanaohjusika kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia taratibu zilizokubalwia na wadau", amesema Rais Samia Suluhu Hassan.
Kabla ya uchaguzi wa leo wa serikali za mitaa, baadhi ya vyama vya upinzani vilitoa malalamiko kuhusu "taratibu zisizokubalika" ambazo vinadai ziliandamana na kampeni za uchaguzi huo.
Msemaji wa chama cha ACT Wazalendo anayehusika na masuala ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Rahma Mwita amelaani vikali matukio ya kutekwa, kukamatwa, na kutishiwa kwa viongozi wa chama hicho saa chache kabla ya uchaguzi.
Kiongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alidai kuwa karibu asilimia 70 ya wagombea wake walienguliwa, mara nyingi kwa sababu za kiutawala kama vile fomu kutokamilika vizuri au kukosa mihuri.
Akitoa takwimu za wagombea, Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa alisema kuwa, nafasi za wenyeviti (mitaa, vijiji na vitongoji) zinazowaniwa ni 80,430 na kwamba upinzani una wagombea 30,977, sawa na asilimia 38.