Sababu na malengo ya utawala wa Kizayuni ya kutishia kuishambulia Iraq
(last modified Tue, 26 Nov 2024 02:28:03 GMT )
Nov 26, 2024 02:28 UTC
  • Sababu na malengo ya utawala wa Kizayuni ya kutishia kuishambulia Iraq

Baada ya mauaji ya kimbari huko Gaza na jinai dhidi ya Lebanon na pia mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya Syria, hivi karibuni utawala wa Kizayuni umeitishia kuishambulia kijeshi Iraq.

Gideon Sa'ar Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Utawala wa Kizayuni wa Israel amempatia barua Mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambapo ndani yake ametaka achukue hatua za haraka kuhusiana na harakati za makundi ya Iraq yanayotumia ardhi ya nchi hiyo kufanya mashambulizi dhidi ya ardhi za Palestina zinazokaliwa (Israel).

Mbali na kuwasilisha malalamiko hayo kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kupinga operesheni za makundi ya muqawama ya Iraq dhidi ya Israel yanayounga mkono Lebanon na Ukanda wa Gaza, utawala huo wa Kizayuni umeitishia kuishambulia kijeshi Iraq.

Madai ya utawala wa Kizayuni dhidi ya makundi ya muqawama ni kwamba makundi hayo yamekiuka mamlaka yake ya kujitawala kwa kuushambulia mara kwa mara utawala huo. Kuhusiana na hili, makundi ya "Kataib Hizbullah", "Asaib Ahl al-Haq", "Al-Nujba", "Kataib Seyyed Al-Shahada", "Ansar Allah Al-Awfia" na "Badr" ni makundi ya muqawama ya Kiislamu ya Iraq ambayo Israel imeyataja katika barua iliyoituma kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuyatambulisha kuwa ni malengo yake nchini Iraq.

Lengo la utawala wa Kizayuni la kuitishia Iraq kwa mashambulizi ya kijeshi ni kuzuia makundi ya muqawama kuendelea na mashambulizi dhidi ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu. Hata hivyo, viongozi wa muqawama wanasisitiza kuwa, hata mashambulizi ya kijeshi hayatazuia mashambulizi dhidi ya maeneo yanayokaliwa kwa mabavu kwa sababu makundi hayo yanaona ulinzi wa Gaza ni wajibu wao wa kiutu na kibinadamu.

 

Kuhusiana na suala hilo, mmoja wa viongozi wa harakati ya Al-Nujba ya Iraq amesema kuwa, muqawama wa Iraq hautaacha wajibu wake wa kimaadili na kitaifa katika kuziunga mkono Lebanon na Palestina na kuushambulia kwa nguvu zote utawala wa Kizayuni. Ni kichekesho kwamba Israel inalalamika; huku kila siku ikitenda uhalifu wa kutisha sana dhidi ya ubinadamu.

Lengo jingine la utawala wa Kizayuni la uwezekano wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya makundi ya muqawama ya Iraq ni kudhoofisha mhimili wa muqawama ambayo ndio sera kuu ya utawala huo. Lengo hili sasa linafuatiliwa nchini Lebanon, Palestina na Syria.

Hata hivyo, suala muhimu ni kwamba hatua ya kijeshi iliyochukuliwa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iraq inaweza kuwa na matokeo muhimu kwa Marekani. Kuna vituo muhimu vya kijeshi vya Marekani nchini Iraq na makundi ya muqawama yanaweza kwa urahisi kabisa kuvifikia na kuvilenga kwa mashambulio.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

 

Kwa muktadha huo, hofu ya Washington ya majibu ya kulipiza kisasi ya makundi ya muqawama wa Kiislamu ya Iraq dhidi ya kambi za Marekani huko Iraq na mipakani mwa Syria imeifanya Washington kushikwa na kigugumizi cha kutoa ridhaa ya kufanyika mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iraq.

Wakati huo huo, uungaji mkono wa Marekani kwa uwezekano wa kuchukuliwa hatua za kijeshi na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iraq unaweza kuandaa uwanja wa  kuibuka upinzani wa fikra za waliowengi dhidi ya Marekani na kuongeza matakwa ya kufukuzwa wanajeshi wa Marekani kutoka katika ardhi ya Iraq.