Kukata tamaa kwa utawala wa Kizayuni dhidi ya makundi ya muqawama
Licha ya uungaji mkono wa pande zote wa Ikulu ya White House kwa Tel Aviv, utawala wa Kizayuni hauna uwezo wa kukabiliana na makundi ya muqawama ya Palestina na Hizbullah ya Lebanon katika vita hivyo.
Huku vita vikiendelea huko Ukanda wa Gaza, na oparesheni za Hizbullah nchini Lebanon kusababisha uharibifu mkubwa kwa jeshi, vituo vya usalama na kijasusi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel), wakuu wa utawala wa Kizayuni na makamanda wa kijeshi wa utawala huo wanakiri kushindwa kwao kukabiliana na hali hiyo pamoja na makundi ya muqawama.
Gazeti la Kizayuni la Haaretz, likiwanukuu maafisa wa zamani wa Israel, limeripoti kuwa Benjamin Netanyahu, ambaye hakuwa akitambua mipaka yoyote, ameingiwa na hofu kubwa na sasa anauelekeza utawala wa Israel kwenye shimo la kuzimu. Likinukuu vyanzo vya habari, limeandika kwamba, Netanyahu amevuruga makubaliano ya kubadilishana mateka na Hamas mara tatukatika miezi michache iliyopita. Katika kujibu kashfa ya kiusalama na taarifa zilizovujishwa kutoka ofisini kwake, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni pia amesema: "Kuvuja kwa taarifa hizi ni tishio kubwa kwa usalama wa Israel."
Mgogoro wa usalama katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Israel umekuwa ikichukua mwelekeo mpya siku hadi siku, na sasa watu wanaomzunguka Netanyahu na wanachama wa ofisi yake wameshutumiwa kwa kuvujisha taarifa za siri. Mbali na kushindwa mfululizo jeshi la Kizayuni na jmakundi ya muqawama, kufichuliwa taarifa za siri kutoka ofisi ya Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni imekuwa kashfa nyingine kwa Netanyahu ambaye anakabiliwa na shutuma kali kutoka kwa vyama vya upinzani vya utawala huo.
Mbali na kashfa ya usalama ya Netanyahu, na katika upande wa vita hususan dhidi ya Hizbullah ya Lebanon, jeshi la utawala wa Kizayuni halina uwezo wa kukabiliana na muqawama wa Lebanon. Hizbullah ya Lebanon inaendelea kufanya operesheni zake kwa mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali, huku Wazayuni wakikiri kutokuwa na uwezo wa kupambana nayo.
Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umetangaza kuwa, mapema Jumamosi tarehe 23, kulifanyika oparesheni 34 za kijeshi dhidi ya utawala wa Kizayuni, operesheni ambazo zilijumuisha juhudi za vikosi vya muqawama za kuzuia kusonga mbele jeshi la Kizayuni na kushambulia vikosi hivyo katika maeneo ya mpaka wa Lebanon na ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo haramu wa Israel.
Hii ni katika hali ambayo Jenerali Michael Eric Kurila, Kamanda wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) alikutana mjini Tel Aviv na Herzi Hallivy, Mkuu wa Jeshi la utawala wa Kizayuni ambapo wawili hao walifanya tathmini ya pamoja ya hali ya usalama kaskazini mwa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu (Israel) ambayo lengo lake kuu lilikuwa kujadili na kutathmini masuala ya kimkakati ya usalama, hasa kuhusiana na Lebanon.
Matukio ya eneo katika siku za hivi karibuni yamefichua kuwa, utawala wa Kizayuni umekuwa hatarini mno kutokana na kupanuka vita, ambapo vikosi vya muqawama vimelenga kwa urahisi vituo nyeti vya kijeshi na kiusalama na kijasusi vya utawala wa Kizayuni katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo pandikizi.
Mbinu ya uendeshaji vita ya Hezbollah nchini Lebanon, imeweka wazi mgogoro wa kiusalama wa Tel Aviv ambapo kuendelea vita kumedhihirisha wazi udhaifu wa utawala huo na kuwafanya makamanda wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni kutoa onyo kali kuhusu matokeo ya kuendelea kwa vita na taathira zake mbaya katika siku zijazo.
Mgogoro wa usalama wa Tel Aviv leo ni matokeo ya vita vinavyoendelea huko Ukanda wa Gaza na Lebanon. Netanyahu na mawaziri wake wenye misimamo ya kufuru ada hawana hoja zozote za kuhalalisha hatua zao, ambapo vyama vya upinzani vya utawala wa Kizayuni vinalichukulia baraza la mawaziri kuwa chanzo kikuu cha mgogoro unaoukabili utawa huo. Utawala haramu wa Kizayuni haujawahi kukabiliwa tena na hali kama hiyo na kudhoofika kwake kiusalama na kijeshi katika vita na makundi ya muqawama kumepelekea kuporomoka kisiasa, kiuchumi na kiusalama kwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel).