Araghchi: Jamhuri ya Kiislamu inaunga mkono mazungumzo ya kustawisha amani
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu yenye utamaduni na ustaarabu tajiri na wa muda mrefu, ni muungaji mkono na mlinganiaji wa maingiliano na mazungumzo ya kuhimiza amani na kuishi pamoja baina ya nchi mbalimbali.
Sayyid Abbas Araghchi jana Jumanne alieleza misimamo ya Iran kuhusu suala la amani na maendeleo ya kikanda katika mkutano wa 10 wa Muungano wa Ustaarabu wa Umoja wa Mataifa nchini Ureno na kuashiria maafa ya binadamu yaliyosababishwa na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya watu wa Palestina. Vilevile amekosoa utepetevu wa taasisi za kimataifa katika miezi 14 ya jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema jinai na ukatili wa utawala wa Kizayuni vimeiweka jamii ya kimataifa mbele ya mtihani mzito, na taasisi za kimataifa kama vile Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, zimeshindwa kutimiza wajibu wao wa kimsingi mbele ya ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa na haki za binadamu.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameeleza kuwa ni jambo lisilowezekana kuimarisha amani na utulivu duniani bila ya kutilia maanani maafa ya binadamu ya hivi sasa eneo la Asia Magharibi na kusema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya njama za kuliangamiza taifa la Palestina kwa miongo kadhaa iliyopita. Amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inatakiwa kuchukua hatua za haraka na za pamoja ili kukomesha mpango huo wa kikoloni na wa kibaguzi, na kwamba Marekani na nchi nyingine zinazotoa misaada ya kijeshi na kisiasa kwa utawala wa Israel zinahesabiwa kuwa washirika wake na zinapaswa kuwajibika.
Araghchi amelaani utumiaji mbaya na wa muda mrefu wa madai ya "chuki dhidi ya Uyahudi" unaofanywa na viongozi wa utawala ghasibu wa Israel kwa ajili ya kunyamazisha ukosoaji na maandamano yoyote dhidi ya siasa za jinai za Israel na kusisitiza kuwa, kupatikana amani katika eneo la Magharibi mwa Asia kunahitaji kutimizwa haki ya kujitawala watu wa Palestina na kukomeshwa uvamizi na utawala wa kibaguzi wa Israel.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran aidha ametaka kutekelezwa kikamilifu amri za Mahakama ya Kimataifa ya Uadilifu kuhusu kukabiliana na mauaji ya kimbari huko Palestina na pia kutekelezwa mara moja hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ya kukamatwa Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu.