Iran: Ushindi wa Trump ni fursa kwa Marekani kurekebisha 'sera zisizo sahihi'
Iran inasema itaihukumu serikali mpya ya Marekani kwa misingi ya sera na mienendo yake baada ya Donald Trump kushinda uchaguzi wa rais siku ya Jumatano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alisema jana Alkhamisi kwamba ushindi wa Trump katika uchaguzi wa rais ni fursa kwa Marekani kutathmini upya "sera zake mbovu" za huko nyuma.
Mwaka 2018, na chini ya rais wa wakati huo, Donald Trump, Marekani ilijiondoa kwa upande mmoja katika mapatano ya nyuklia yaliyotiwa saini mwaka 2015 na kuiwekea Jamhuri ya Kiislamu msururu wa vikwazo vikali.
"Tuna uzoefu mchungu sana na sera na mienendo ya serikali tofauti za Marekani katika miaka ya huko nyuma," Amesema Esmaeil Baghaei katika mahojiano yake na shirika la habari la IRNA.
Ameongeza kuwa, matokeo ya "uchaguzi huo ni fursa ya kuchunguza na kurekebisha mienendo isiyo sahihi ya zamani ya serikali ya Washington."
Baghaei amesisitiza msimamo wa awali wa Iran kwamba matokeo ya uchaguzi wa rais nchini Marekani hayana tija kwa Jamhuri ya Kiislamu.
"Kazi ya kuchagua rais wa Marekani ni jukumu la watu wa nchi hiyo, na sasa Wamarekani wamefanya chaguo lao," amesema Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na kuongeza kuwa: "Kilicho muhimu kwa Iran ni utendaji wa serikali ya Marekani."
Kabla ya hapo, Msemaji wa Serikali ya Iran, Fatemeh Mohajerani aliwaambia waandishi wa habari mjini Tehran kwamba Iran haioni tofauti yoyote kati ya Trump na mpinzani wake wa chama cha Democratic, Kamala Harris.
"Kimsingi, hatuoni tofauti yoyote kati ya watu hawa wawili [Trump na Harris]. Vikwazo vimeimarisha nguvu ya ndani ya Iran na tuna uwezo wa kukabiliana na vikwazo vipya," amesema Fatemeh Mohajerani.