2024 huenda ukawa mwaka wa joto zaidi kuwahi kurekodiwa duniani
Mwaka huu wa 2024 uko mbioni kuwa mwaka wa joto zaidi kuwahi kutokea duniani. Haya ni kwa mujibu wa shirika la hali ya hewa la Ulaya, Copernicus.
Taarifa ya shirika hilo imesema, mwaka huu pia huenda ukawa wa kwanza wa kuwa na zaidi ya nyuzi joto 1.5 au nyuzi joto 2.7 kwa kipimo cha Selsiasi kuliko nyakati za kabla ya viwanda.
Rekodi za Marekani, Uingereza na Japani zinazoanza katikati ya karne ya 19, zinaonyesha kuwa muongo uliopita ulikuwa wa joto zaidi tangu vipimo vya kawaida vianze kuchukuliwa, na kuna uwezekano katika miaka 120,000, kulingana na badhi ya wanasayansi.
Taarifa ya shirika la hali ya hewa la Ulaya, Copernicus imesema: Ingawa mwaka wa 2024 umekuwa wa joto sana, kilichosababisha msimu huu wa kiangazi kuingia katika eneo jipya ni msimu wa baridi uliokuwa na joto kuliko kawaida wa Antaktika. Jambo hilo hilo lilitokea katika ncha ya kusini mwaka jana wakati rekodi hiyo ilipowekwa mapema mwezii Julai.
Wanasayansi wa hali ya hewa wanasema rekodi nyingi za kupanda kiwango cha joto hutokana na shughuli za binadamu ambazo huzalisha hewa ya kaboni dioksidi na methane.
Mazungumzo ya mwaka huu ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa yatalenga hasa jinsi ya kufadhili mabadiliko katika masuala ya nishati na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.
Shirika la Hali ya Hewa Duniani lilisema mataifa mengi ya Afrika yanatumia hadi 9% ya bajeti zao kwa sera za kukabiliana na hali ya hewa.