Iran na Angola zalaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel
Balozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Angola na rais wa nchi hiyo wamelaani vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.
Mansour Shakib-Mehr, balozi asiye mkazi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Angola amepongeza misimamo ya serikali ya Luanda katika kuulaani utawala wa Kizayuni.
Shakib Mehr amesema katika hafla rasmi ya kuwasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais wa Angola, João Lourwnco, iliyofanyika katika ikulu ya Luanda, kwamba, ana matumaini kama ambavyo nchi zote na jamii ya kimataifa, zilisimama dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi nchini Kusini Afrika, zitasimama pia dhidi ya ubaguzi wa rangi na mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel.
Balozi asiye mkazi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Angola pia amefikisha salamu za Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Rais wa Angola na kutoa wito wa kuendelezwa uhusiano wa pande mbili katika nyuga zote hususan sekta za kiuchumi na kibiashara.
Kwa upande wake Rais Joao Lourenco wa Angola amesisitiza kuwa: Tunalaani mashambulizi haya ya Israel na tunaamini kwamba amani na usalama vinapaswa kudumishwa katika eneo hilo na Israel inapaswa kukomesha mashambulizi yake.
Akizungumzia ulazima wa kuunda taifa huru la Palestina, Rais wa Angola alidokeza kuwa nchi yake inaunga mkono kikamilifu suala hilo.