Rais Pezeshkian: Mazungumzo kati ya Wasyria wote ni muhimu ili kufikia muafaka
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i119912-rais_pezeshkian_mazungumzo_kati_ya_wasyria_wote_ni_muhimu_ili_kufikia_muafaka
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema kuwa makundi yanayopingana nchini Syria yanapaswa kufungua mazungumzo ili kufikia makubaliano kuhusu uongozi wa kisiasa wa nchi hiyo baada ya wanamgambo kuchukua udhibiti wa Damascus.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Dec 09, 2024 04:39 UTC
  • Rais Pezeshkian: Mazungumzo kati ya Wasyria wote ni muhimu ili kufikia muafaka

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian anasema kuwa makundi yanayopingana nchini Syria yanapaswa kufungua mazungumzo ili kufikia makubaliano kuhusu uongozi wa kisiasa wa nchi hiyo baada ya wanamgambo kuchukua udhibiti wa Damascus.

Rais wa Iran alitoa kauli hiyo kwenye hotuba katika kikao cha baraza la mawaziri Jumapili kufuatia kuanguka kwa serikali ya Syria baada ya makundi ya wapiganaji yanayoongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) kuingia Damascus.

Alisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, mamlaka ya kitaifa na mipaka ya Syria. Alionyesha matumaini kwamba migogoro ya kijeshi na vurugu zitaisha nchini Syria mapema iwezekanavyo "ili watu wa Syria waweze kuamua hatima yao wenyewe katika mazingira ya utulivu yasiyo na vurugu, wasiwasi au uingiliaji wa nje mbaya."

Pezeshkian amesisitiza umuhimu kuhakikisha usalama wa raia wote wa Syria na wageni na kulinda maeneo matakatifu naa ofisi za kidiplomasia kulingana na sheria za kimataifa.

Aliongeza kwamba Iran itaendelea na mashauriano yake ya kidiplomasia na pande zote husika pamoja na Umoja wa Mataifa kusaidia kuboresha hali nchini Syria na kuimarisha utulivu na usalama katika eneo hilo.

Rais wa Iran alikosoa vikali uvamizi wa utawala wa Kizayuni Israel dhidi ya eneo la Syria na ametoa wito kwa pande zote katika nchi hiyo ya Kiarabu na mataifa jirani kukaa macho kwani utawala huo wa Kizayuni unalenga  kutumia vibaya hali ya Syria ili kuendeleza malengo yake ya kujitanua na yasiyo halali.