Spika Qalibaf: Iran itaheshimu uamuzi wowote utakaochukuliwa na watu wa Syria
Spika wa Bunge la Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu inaheshimu uamuzi wowote utakaochukuliwa na wananchi wa Syria na itaendelea kufuatilia mienendo na sera zake.
Qalibaf amesema hayo katika mkutano na wanafunzi wa chuo kikuu mjini Tehran baada ya makundi ya wanamgambo, yanayoongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), kuuteka mji mkuu wa Syria.
Amesema Iran inafuatilia utendaji wa serikali ya Syria, na itashirikiana nayo kwa sharti kwamba haifuati kundi la Daesh (ISIS), haishirikiani na Wazayuni na inalenga kuimarisha umoja wa Umma wa Kiislamu.
Spika wa Bunge la Iran amesema, wakati wa hujuma za kundi la kigaidi la Daesh, Jamhuri ya Kiislamu ilijibu ombi la serikali za Syria na Iraq na kupigana na matakfiri hao.
"Nitasema kwa uwazi: Shahidi Soleimani alimwambia mara kwa mara Bashar al-Assad kwamba unapaswa kuwa makini na watu wako; Kwa sababu, mbali na magaidi wa ISIS, kulikuwa na makundi kadhaa ya wapinzani wenye silaha ambayo yalijadiliwa hata kwenye mkutano wa Astana." "Hatuna kazi yoyote na makundi ya upinzani huko Syria na tatizo letu lilikuwa na magaidi wa ISIS", amesisitiza Spika Qalibaf.
Amesema kuwa Iran inaheshimu uamuzi wowote unaochukuliwa na watu wa Syria na itachukua hatua kwa mujibu wa mienendo ya serikali itakayoundwa nchini Syria.
Qalibaf ameongeza kuwa: Wazayuni na Marekani bado wanaendeleza njama na mipango yao na kamwe hawatasimamisha uadui wao dhidi ya Uislamu.