Ayatullah Jannati: Marekani na washirika wake lazima wawajibike kuhusu Syria
Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Marekani na waitifaki wake wanapaswa kuwajibishwa kuhusiana na matukio ya Syria.
Ayatullah Ahmad Jannati, amesema hayo leo mwanzoni mwa kikao cha Baraza la Kulinda Katiba ya Iran kuhusiana na matukio ya eneo hili na kubainisha kwamba: Utawala wa Kizayuni wa Israel katika masiku haya unatumia vibaya hali ya Syria na kufanya mashambulizi dhidi ya miundombinu ya nchi hiyo hatua ambayo ni uhalifu wa kibinadamu, ambao madhara yake yataathiri watu wa nchi hiyo kwa miaka mingi.
Katibu wa Baraza la Kulinda Katiba ya Iran amesema: "Utumiaji mbaya wa hali ya Syria unaofanywa na utawala wa Kizayuni hivi sasa ni jinai kubwa."
Ayatullah Jannati ameongeza kuwa, kuwashambulia watu wasio na ulinzi ni mbinu ya kawaida ya viongozi wahalifu wa utawala wa Kizayuni na kubainisha kwamba, uungaji mkono wa Marekani na washirika wake ndio kichocheo bora zaidi kwa utawala huu haramu, na lazima wawajibike kwa ubinadamu na watu wa eneo.
Ayatullah Jannati amesema: Marekani, ambayo inajionyesha kama mtetezi mkuu wa haki za binadamu, kwa hakika ndiyo mkiukaji mkubwa zaidi wa haki za binadamu ulimwenguni.