Ndege ya mizigo iliyotengenezwa Iran yafanyiwa majaribio
Ndege nyepesi ya mizigo ya Iran, iliyopewa jina la Simorgh, ambayo imeundwa kikamilifu na wataalamu wa Kampuni ya Utengenezaji Ndege ya Iran (HESA), imefanyiwa majaribio yaliyofana, baada ya kufanyiwa ukaguzi mbalimbali ili kupokea cheti cha kuraka.
Ndege hiyo ya mizigo ya kijeshi ya muundo wa turboprop, ilifanyiwa majaribio siku ya Jumatano wakati wa toleo la 12 la Maonyesho ya Kimataifa ya Anga ya Iran, ambayo pia yanajulikana kama Iran Airshow 2024, ambayo yamefanyika kwenye Kisiwa cha Kish kaskazini mashariki mwa Ghuba ya Uajemi.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Ulinzi wa Iran Brigedia Jenerali Amir Nasirzadeh alisema: "Ndege hii imeundwa kwa kufuata viwango na kanuni za kimataifa." Amesema ndege hiyo imenduwa na wataalamu wa Wizara ya Ulinzi kwa kushirikiana na makampuni mengine ya kiteknlojia ya ndani ya nchi.
Brigedia Jenerali Nasirzadeh ameashiria maendeleo yaliyopatikana katika nyanja za kiulinzi na kijeshi nchini Iran na kusema kuwa, mafanikio makubwa katika sekta ya usafiri wa anga yamefikiwa katika miaka michache iliyopita, na hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu inaweza kuzalisha aina mbalimbali za zana za kisasa za kijeshi.
Mkuu huyo wa Ulinzi wa Iran ameendelea kubainisha kuwa Iran imefanikiwa kujitosheleza katika sekta ya usafiri wa anga, akisisitiza kuwa vikwazo vya nchi za Magharibi "havijaweza kudhoofisha nguvu na uwezo wa Iran."
Wataalamu na wahandisi wa kijeshi wa Iran katika miaka ya hivi karibuni wamefikia mafanikio makubwa katika utengenezaji wa aina mbalimbali za zana za kijeshi, na kufanya majeshi ya Iran yafikie kiwango cha kujitosheleza.
Iran sasa ni miongoni mwa nchi chache duniani zinazomikili teknolojia muhimu za kuunda zana zote za kivita ambazo zinahitajiwa na majeshi. Madola ya Magharibi yaliiwekea Iran vikwazo ili isiweze kuagiza zana za kivita katika soko la kimataifa lakini Iran iligeuza vikwazo hivyo kuwa fursa ya kujiimarisha na hivi sasa si tu kuwa nchi hii haiagizi zana za kivita kutoka nje ya nchi bali sasa ni muuzaji wa zana hizo katika nchi mbali mbali duniani.