Zaidi ya Wasudan 1,000 warejea nyumbani kwa hiari kutoka Misri
-
Zaidi ya Wasudan 1,000 warejea nyumbani kwa hiari kutoka Misri
Jumla ya raia 1,174 wa Sudan wamerejea nchini kwa hiari wakitokea Misri, ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazoendelea kufanywa na Sudan za kuwarejesha nyumbani raia wake wanaotaka kurejea kutoka nje ya nchi.
Shirika la Habari la Sudan (SUNA limeripoti kuwa Kamati Inayosimamia Zoezi la Kuwarejesha kwa hiari nchini Wasudan limeandaa mabasi 24 kwa ajili ya kuwasafirisha Wasudan 1,174 kutoka Misri hadi Sudan.
Zoezi hilo limefadhiliwa na Sekretarieti Kuu ya Baraza la Zaka la Sudan ambayo ni chombo cha serikali na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu wake, Yahya Ahmed Al-Qamrawi.
Shirika la habari la Sudan SUNA limemnukuu Mohamed Wadaa, Mkuu wa Kamati Inayosimamia Zoezi la Kuwarejesha nchini kwa hiari raia wa Sudan akieleza kuwa kamati hiyo imejitolea kuendelea na juhudi za kuwarudisha watu nyumbani Wasudan ili kuhakikisha kuwa yoyote anayetaka kurudi kwa hiari anarajea nchini.
Katika zoezi hilo, Sudan imetoa kipaumbele kwa wagonjwa na wazee ambao wanarejea Sudan kwa kutumia njia mbalimbali za usafiri ikiwemo usafiri wa anga.
Mapema jana Jumamosi, Waziri Mkuu wa Sudan, Kamil Idris alisisitiza tena uungaji mkono wake kwa zoezi hilo la kurejea kwa hiari raia wa nchi hiyo kutoka nchi zilizowapa hifadhi.
Kwa mujibu makadirio rasmi ya serikali, zaidi ya Wasudan milioni 1.2 walikimbia Misri tangu kuzuka vita vya wenyewe kwa wenye nchini Sudan mwezi Aprili 2023.
Kabla ya kuanza vita nchini Sudan, Misri ilikuwa imewapokea wakimbizi wa Kisudan milioni 5.
Vita vya kuwania madaraka kati ya jeshi la Sudan na wanamgmbo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) vilivyoanza Aprili vimesababisha kushuhudiwa mojawapo ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani, ambapo hadi sasa makumi ya maelfu ya watu wameuawa na wengine wasiopungua milioni 13 wamelazimika kuwa wakimbizi kutokana na vita hivyo.