Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Wavamizi watatimuliwa Syria
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i120098-khatibu_wa_swala_ya_ijumaa_tehran_wavamizi_watatimuliwa_syria
Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria matukio ya Syria na kusema muqawama utaimarika na kuwatimua waliovamia ardhi ya Syria na kuikalia kwa mabavu.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 13, 2024 06:51 UTC
  • Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran: Wavamizi watatimuliwa Syria

Khatibu wa Swala ya Ijumaa mjini Tehran ameashiria matukio ya Syria na kusema muqawama utaimarika na kuwatimua waliovamia ardhi ya Syria na kuikalia kwa mabavu.

Ayatullah Sayyid Ahmad Khatami Khatibu na Imamu wa Swala ya Ijumaa wiki hii mjini Tehran amesema: "Kinara wa kundi lililotwaa madaraka nchini Syria, amesema wazi kwamba hana nia ya kuanzisha vita dhidi ya Israel."

Akijibu kauli hiyo, Khatibu wa Swala ya Ijumaa Tehran amesema inajulikana vyemba kwamba kinara wa kundi hilo lililonyakua madaraka Syria ni kibaraka wa utawala wa Kizayuni wa Isral na kwamba utawala wa Kizayuni ulimsaidia.

Ayatullah Khatami ameendelea kwa kusema: "Ninaiambia Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, nchi za Asia Magharibi na Saudi Arabia, Misri na Jordan kwa uwazi kwamba, utawala wa Kizayuni wa Israel umetumia vibaya fursa ya hali iliyojitokeza kuikalia zaidi Syria na kuharibu miundombinu yote ya nchi hiyo."

Amesema lengo la utawala wa Kizayuni ni kunyakua ardhi zote za nchi za Kiarabu kutoka Mto Nile hadi Euphrates. Amesema utawala wa Kizayuni ukiimarika, utazifuata nchi hizo za Kiarabu na hivyo zinapaswa, "kumsitisha mbwa huyu mwenye kichaa bila kuchelewa."

Halikadhalika amesema utawala wa Kizayuni ni tishio kwa usalama wa kimataifa, na jamii ya kimataifa inapaswa kuchukua hatua za kuuzuia

Ayatullah Khatami amesema: "Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amebainisha matumaini kuwa vijana wa Syria watainuka na kuiokoa nchi yao, na Mwenyezi Mungu akipenda, vijana wa Syria watajitokeza na kukwamisha mipango ya Marekani na utawala wa Kizayuni."

Akiendelea na hotuba yake, Ayatullah Khatami amesema inapaswa kufahamika kuwa hata baada ya matukio ya Syria muqawama haujadhoofika na wala Iran ya Kiislamu haijadhoofishwa.

Aidha amesema kwa miaka 45 sasa tangu Mapinduzi ya Kiislamu yapate ushindi nchini Iran maadui wamejaribu kutekeleza kila aina ya njama dhidi ya nchi hii lakini wamefeli.