Waziri wa Afya: Iran ni kinara wa kikanda katika dawa za nyuklia
Waziri wa Afya, Tiba na Elimu ya Tiba wa Iran, Mohammad Reza Zafarqandi ametangaza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ndio kinara wa kanda ya Asia Magharibi katika masuala ya nyuklia na kubainisha kuwa, kuna vituo 220 vya dawa za nyuklia katika maeneo mbalimbali ya nchi vinavyonufaika na uwezo huo na malighafi zinazozalishwa na Shirika la Atomiki la Iran.
Zafarqandi amesema haya katika mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran, Muhammad Eslami. Amongeza kuwa: Shughuli za Shirika la Atomiki na Sekta ya Nyuklia katika nyanja ya afya, matibabu na elimu ya matibabu zinastahiki kupongezwa na limepata mafanikio makubwa sana kwa kutumia teknolojia za kisasa.
Ameongeza kuwa: Kwa ujumla, kazi mbili muhimu sana zimekamilika katika shirika hili, moja katika uwanja wa uchunguzi wa magonjwa na nyingine katika uwanja wa matibabu. "Katika uwanja wa utambuzi wa magonjwa, shirika hili limetekeleza mbinu nyingi za kisasa za uchunguzi kama vile PET-Scan ya malighafi na cyclotron. Na katika uwanja wa matibabu, Shirika la Atomiki la Iran linakabidhi dawa nyingi kwa vituo vya matibabu ya dawa za nyuklia," amesema Zafarqandi.
Waziri wa Afya wa Iran amesema: Ili kutekeleza mipango na miradi katika nyanja za matibabu kwa uhakika zaidi, tunaendeleza ushirikiano wetu na Shirika la Atomiki la Iran na matawi yake, ambayo kwa njia hii, yanaweza kutumia maabara, hospitali na vituo vya matibabu, chini ya usimamizi wa Waziri wa Afya.