Iran yahimiza kufanyika juhudi zaidi za pamoja za kukomesha jinai za Israel
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika Masuala ya Kisiasa, Majid Takht Ravanchi amesema kuwa, nchi zote lazima zifanye juhudi za dhati za kukomesha ukatili wa utawala wa Israel na kuwaadhibu viongozi wa utawala huo kutokana na jinai zao za kutisha.
Takht Ravanchi amesema hayo katika mazungumzo yake ya ana kwa ana na Funakoshi Takehiro, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Japan hapa Tehran.
Amesema utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea na vita vyake vya mauaji ya halaiki katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu na umepanua uchokozi wake nchini Syria.
Amesema: Jamii ya kimataifa ina dhima ya kufanya juhudi za pamoja za kuulazimisha utawala wa Kizayuni ukomeshe jinai zake na mauaji ya umati.
Takriban Wapalestina 44,976, wengi wao wakiwa watoto wadogo na wanawake, wameshauawa shahidi na wengine zaidi ya 106,759 kujeruhiwa katika mashambulizi ya kikatili yanayoendelea kufanywa na wanajeshi makatili wa Israel huko Ghaza tangu Oktoba 7, 2023.
Mashambulizi hayo ya kikatili yanafanyika kwa uungaji mkono usio na kikomo wa kijeshi na kisiasa kutoka kwa washirika wa Magharibi wa Israel, zikiwemo Marekani na Ufaransa.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisheria na kimataifa, Kazem Gharibabadi alifanyiwa mahojiano na tovuti ya Khamenei.ir na kusema: "Ni jambo linalowezekana kutolewa adhabu ya kifo kwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutokana na uhalifu na jinai zake za kivita alizowafanyia Wapalestina huko Gaza."