Iran Kurudi Nyuma, Kamwe?
Je, Iran imelegeza kamba na kurudi nyuma? Wakati Donald Trump alipojiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na kuanza kutekeleza sera ya mashinikizo ya juu zaidi dhidi ya Iran, wengi walidhani kuwa Iran ingesalimu amri.
Lakini historia inasema nini? Je, kweli Iran iko tayari kukabidhi uwanja kwa wapinzani wake wenye nguvu zaidi?
Mwezi Aprili 2023, baada ya shambulio la Israel kwenye jengo la ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria, Tehran ilijibu kwa njia ambayo ilikuwa haijawahi kushuhudiwa. Zaidi ya makombora 350 ya balestiki, cruise na ndege zisizo na rubani (drone) yalirushwa dhidi ya Israel. Shambulio hilo lilikuwa la kwanza la moja kwa moja la Iran dhidi ya Israel na lilionyesha kuwa Tehran imehama kutoka katika kutumia diplomasia pekee, hadi kwenye matumizi ya nguvu. Swali linalojitokeza ni kwamba, kwa nini ilifanya hivyo?

Historia inaonyesha kwamba, Iran sio tu kwamba hairudi nyuma na kulegeza kamba kutokana mashinikizo, lakini mara nyingi huwapa changamoto maadui wake kwa mikakati erevu na mashambulizi ya kukabiliana nao. Tangu baada ya kumalizika vita vya Iraq dhidi ya Iran mwaka 1988 hadi kuanguka tawala za Taliban na Saddam Hussein katika miaka ya 2000, Tehran daima imekuwa ikitumia matukio ya kikanda kwa ajili ya kuimarisha nafasi yake. Tuliona mkakati huo huo katika kujibu sera ya mashinikizo ya juu zaidi ya Trump: Badala ya kusalimu amri, Iran iligeukia mashambulizi yasiyo na ulinganifu (asymmetric attacks) na kumtia hasara kubwa adui.
Mnamo Julai 2023, Israel ilichukua hatua ya kijuba na kumuua Ismail Haniyeh, kiongozi wa kisiasa wa harakati ya Hamas, akiwa mjini Tehran. Lakini badala ya kupunguza ushawishi wa Iran, hatua hiyo ilipelekea kuongezeka migogoro na machafuko.
Historia imeonyesha kwamba, hata hatua kama vile mauaji ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani na Israel dhidi ya aliyekuwa kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Qassem Soleimani, hazikuweza kupunguza nguvu na ushawishi wa kikanda wa Iran. Kinyume chake, Iran daima imedumisha nafasi yake kwa kutegemea uwezo wake wa kijeshi na kisiasa.
Lakini, kwa nini sera za Marekani zimekuwa butu na hazifanyi kazi tena kama zamani?
Kwa upande mmoja, China na nchi nyingine zimeifanya mitandao ya kukwepa vikwazo kuwa tata zaidi, na mafuta ya Iran yanaendelea kutiririka katika masoko ya bidhaa hiyo. Kwa upande mwingine, nchi za Ghuba ya Uajemi zilizokuwa zikiunga mkono siasa kali za Marekani, sasa zinapendelea kushirikiana na Iran badala ya kukabiliana nayo.

Mabadiliko haya yamezifanya butu zana za mashinikizo za serikali ya Washington.
Sambamba na mabadiliko haya, kuna ushahidi unaoonyesha kwamba Iran inaweza kuelekea kwenye mabadiliko katika "Mwongozo wake ya Ulinzi". Kwa mara ya kwanza katika miongo miwili iliyopita, maafisa wa Iran wamezungumza waziwazi kuhusu uwezekano wa kuvuka na kuweka kando mipaka waliyojiwekea kuhusiana na masuala ya nyuklia. Je, hii ni ishara ya mabadiliko ya kina katika sera ya ulinzi ya Iran?
Historia ya miaka 45 ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran imeonyesha kuwa, nchi hii haikati tamaa inapokabiliwa na migogoro mikubwa, bali pia inatumia mashinikizo kama fursa, kwa mikakati yake ya kiubunifu.
Je, sera za Marekani na Israel zinaweza kubadilisha mwenendo huo? Na je, Mwongozo wa Sera za Ulinzi za Iran unaelekea kwenye mabadiliko makubwa zaidi?