Sayyid Abbas Araghchi: Bashar Assad alikataa kusikiliza mapendekezo yetu
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Tulitoa mapendekezo mengi kwa Bashar al-Assad, Rais wa zamani wa Syria lakini alikataa kuyasikiliza, tulimtahadharisha kuhusu harakati za upinzani huko Idlib na serikali ya Syria ilifanya maamuzi huru.
Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo akiwa safarini nchini Misri alikokwenda kushiriki katika kikao cha "D-8" katika mahojiano na Televisheni ya "Al-Ghad".
Katika mahojiano hayo, Abbas Araghchi amezungumzia matukio ya hivi karibuni katika Asia Magharibi na pia uhusiano kati ya Iran na Misri.
Sayyid Araghchi amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilikuwepo nchini Syria kwa ombi la serikali ya nchi hiyo kwa lengo la kupambana na makundi ya kigaidi na kamwe haikuingilia mawasiliano na maingiliano ya serikali na wananchi na wapinzani.
Kadhalika, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ameashiria uhusiano wa Misri na Iran na kusema, Cairo na Tehran zina uhusiano wa kihistoria unaoonyesha kuthaminiana juhudi za kila mmoja katika masuala mbalimbali ya kieneo, na kwamba Iran inaunga mkono juhudi kubwa za Misri za kufanikisha usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza.