Stratejia za busara na athirifu za Iran katika kuihami kambi ya muqawama
Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameweka wazi misimamo ya Jamhuri ya Kislamu ya Iran kuhusu matukio ya kikanda na kimataifa. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza hayo katika mahijiano maalumu aliyofanya na mtandao wa Misri wa al Ghad pambizoni mwa mkutano wa wakuu wa nchi za Kiislamu zinazoendelea yaani D-8 mjini Cairo, Misri.
Araqchi ameashiria mpango wa muda mrefu wa Marekani na Wazayuni wa kutaka kuzidhoofisha na kuzigawa vipande vipande nchi kubwa za Kiislamu katika kalibu ya hatua za kujitanua za utawala ghasibu za Israel katika eneo la Mashariki ya Kati na kusisitiza kuwa, vitendo vya utawala wa Kizayuni katika vita huko Gaza na mauaji ya kimbari dhidi ya wanawake, watoto na raia wa kawaida zaidi ya 60,000 huko Gaza na Lebanon, na vilevile mashambulizi ya utawala huo dhidi ya Syria na kuharibiwa miundombinu ya kiulinzi na kiuchumi na ya nchi hiyo vinaonyesha usahihi wa tahadhari za Iran kwamba Israel ni tishio kwa eneo zima la Magharibi mwa Asia.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, lengo kuu la kuasisiwa Mhimili wa Muqawama katika eneo hili ni kupambana na kukabiliana na uvamizi na mashamulizi ya utawala ghasibu wa Israel huko Palestina na kupigania haki za Wapalestina zilizoporwa. Amesema: "Muqawama umetoa vipigo vikali kwa Wazayuni maghasibu licha ya hasara na maafa yaliyoshuhudiwa katika matukio ya baada ya vita vya Gaza na kuuawa shahidi baadhi ya viongozi, na ni vipigo hivyo vikali ndivyo vilivyoulazimisha utawala ghasibu wa Israel kufanya mazungumzo na kukubali usitishaji vita huko Lebanon."
Baada ya kuanza operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa, hali ya mambo katika eneo la Asia Magharibi ilibadilika na makundi ya Muqawama yalikabiliana na Wazayuni kwa nguvu na utayarifu wa hali ya juu. Matukio hayo yalijiri huku Marekani na serikali za nchi nyingine za Magharibi zikiuhami na kuunga mkono utawala wa Tel Aviv kwa pande zote kifedha na kisilaha.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelipa umuhimu mahususi suala la ushirikiano wa kieneo katika siasa zake za nje kwa lengo la kukabiliana na ushawishi wa nchi ajinabi na hatua zao za kuibua hali ya mchafuko na migogoro. Hii ni katika hali ambayo, utawala wa Kizayuni unaendeleza hatua zake za kujitanua na kuzikalia kwa mabavu ardhi za nchi nyingine kwa himaya ya nchi za Magharib; na unahalalisha hatua zake za uvamizi kwa kupuuza maazimio ya Umoja wa Mataifa.
Israel inaendeleza mwenendo wake wa kuibua mivutano; na ni makundi haya ya Muqawama ambayo kwa kuwa kwao macho na kuwa na uwezo wa hali ya juu wa kijeshi, ambayo yameweza kuwalazimisha Wazayuni kukubali kushindwa mbele ya Muqawama. Makundi ya mapambano yanakabiliana kivitendo na Wazayuni kwa ubunifu na kwa uwezo na nguvu walizonazo yenyewe na hayana utegemezi wowote wa kisiasa na kitaasisi kutoka Iran, bali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na makundi hayo zina mitazamo ya pamoja katika kuwaunga mkono wananchi wa Palestina na katika mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni. Utawala wa Kizayuni umelazimika kufanya mazungumzo ya kusitisha mapigano kufuatia kushindwa na makundi ya Muqawama.
Ushawishi wa Iran katika kanda hii ni kwa lengo la kukabiliana na njama za pamoja za utawala wa Kizayuni na Marekani. Matukio ya Palestina na Lebanon yamefichua kuwa, Wazayuni hawaachani na hatua zao za uvamizi na hawasiti kufanya uharibifu na njama yoyote ili kutimiza malengo yao maovu. Lengo kuu la Marekani na utawala wa Kizayuni ni kupora rasilimali za nchi za kanda hii na kuharibu miundombinu ya Lebanon na Palestina na pia Syria.
Sera za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zimejikita katika kurejesha amani na kusitisha vita kwa kuzingatia matukio ya Syria, Lebanon na Palestina. Mchakato huu utatimia pale Wazayuni maghasibu na waungaji mkono wao wa Magharibi watakapositisha hatua zao za kijuba za kuingilia masuala ya ndani ya nchi za kanda hii na kutokuwa kikwazo kwa amani.