Iran inajenga vitengo viwili zaidi katika Kiwanda cha Nyuklia cha Bushehr
Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema kuwa, Jamhuri ya Kiislamu imo katika harakati za kuanzisha kitengo cha pili na cha tatu cha Kinu cha Nyuklia cha Bushehr, kusini mwa Iran.
Mohammed Eslami amesema hayo na kuongeza kuwa: "Kwa kuzingatia sheria zilizopo na kwa kutilia maanani msimamo uliotangazwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, baadhi ya mipango madhubuti imefanywa humu nchini kwa ajili ya kuweka vinu vya nyuklia kwenye ukanda wa pwani wa kusini mwa nchi, yaani katika maeneo ya Bushehr, Khuzestan, Hormozgan na Mikoa ya Sistan na Baluchestan pamoja na kwenye maeneo ya nyanda za kaskazini mwa nchi, kama vile Mkoa wa Golestan.”
Amesema, kituo cha Bushehr ni miongoni mwa vituo vyenye "uwezo wa hali ya juu" na ni katika mafanikio makubwa ya Jamhuri ya Kiislamu katika sekta ya uzalishaji nishati. Kituo hicho kimesaidia kupunguza gharama za nishati kwa taifa kutokana na kupunguza matumizi ya mapipa milioni 105.7 ya mafuta.
Eslami aidha amesema: "Katika miaka ya hivi karibuni kituo cha nyuklia cha Bushehr cha Iran kimepata maendeleo makubwa. Kimezalisha takriban kilowati 7,400,000,000 za umeme wa nyuklia."
Vilevile amesema: "Mwaka huu ni mwaka wa 50 wa tangu kuanzishwa shirika la nyuklia la Iran." Ameongeza kwamba, kuna sehemu nyingi za sekta ya nyuklia ambazo hadi sasa hazijaguswa wala kufikiwa.