Araghchi: Tutashirikiana na serikali mpya ya Lebanon
(last modified Sat, 11 Jan 2025 10:55:31 GMT )
Jan 11, 2025 10:55 UTC
  • Araghchi: Tutashirikiana na serikali mpya ya Lebanon

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewapongeza wananchi wa Lebanon kwa kupata rais mpya na kusema: Tutashirikiana na serikali yoyote itakayowakilisha matakwa ya wananchi wa Lebanon.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Tasnim, Sayyid Abbas Araghchi ameandika ujumbe katika mtandao wa kijamii kwa ajili ya wananchi wa Lebanon na serikali ya nchi hiyo akisema: Hongera Rais Joseph Aoun na wananchi wapendwa wa Lebanon. Iran inaunga mkono Lebanon iliyo imara, salama na huru. Inaungwa mkono kila nyuma wa Mlebanon kuwa salama isiyo na uvamizi wala vitisho vya kigeni.

Katika ujumbe huo uliochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa X, Sayyid Araghchi amesema: Kama ilivyokuwa zamani, tutashirikiana na serikali yoyote ambayo inawakilisha matakwa ya wananchi wa Lebanon, kuwahakikishia ustawi wao na kulinda mamlaka, uhuru na uadilifu wa maeneo yote ya Lebanon.

Siku ya Alkhamisi, Januari 9, wabunge wa Lebanon walimchagua Joseph Aoun, kamanda wa jeshi la Lebanon, kuwa rais mpya wa nchi hiyo.

Jenerali Joseph Aoun, mwanajeshi mashuhuri wa Lebanon, ambaye amekuwa kamanda wa jeshi la nchi hiyo tangu mwaka 2017, ameweza kuweka jina lake katika orodha ya marais wa nchi hiyo na kuwa rais wa 14 wa Lebanon.