Kamanda wa Kikosi cha Quds: Kipigo kikubwa zaidi dhidi ya Israel kimeonekana
Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (SEPAH) amesema kuwa, kuanza utekelezaji wa usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza kumedhihirisha pigo na kushindwa zaidi kwa utawala wa Kizayuni kutadhihirika.
Brigedia Jenerali Ismael Qaani, Mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya nchini Iran SEPAH amesema hayo katika radiamali yake kwa makubaliano ya usitishaji vita katika Ukanda wa Gaza na kueleza kwamba, Wazayuni wauaji na wafyonzaji damu za watoto wamelazimika kukubali usitishaji vita katika kilele cha udhalili baada ya miezi 15 ya jinai zisizo na kikomo walizotekeleza dhidi watu wanaodhulumiwa wa Palestina, Lebanon na eneo hili.
Kamanda Qaani amesisitiza kwamba, utekelezaji wa makubaliano ya usitishaji vita huko Gaza ni pigo kubwa kabisa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaopata himaya na uungaji mkono wa madola ya Magharibi yakiongozwa na Marekani.
Baada ya ukiukaji wa mara kwa mara wa usitishaji vita uliofanywa na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar ilitangaza jana Jumapili kuwa, makubaliano ya usitishaji vita yameingia katika awamu ya utekelezaji.
Jumatano, Januari 15, 2025, Serikali ya Qatar ilitangaza kupatikana mafanikio ya juhudi za kusimamisha mapigano katika Ukanda wa Ghaza kati ya pande za Palestina na Israel, na kwamba utekelezaji wa makubaliano hayo utaanza kutekelezwa leo (Jumapili, Januari 19) ili kuhitimisha miezi zaidi ya15 ya vita vya kinyama na mauaji ya kimbari ya zaidi ya watu 46,000 yaliyofanywa na jeshi la Kizayuni.