Araqchi amjibu Guterres: Ni kukosa adabu kuwapa mawaidha Wairani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121808-araqchi_amjibu_guterres_ni_kukosa_adabu_kuwapa_mawaidha_wairani
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu matamshi yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akisisitiza kuwa Iran haijawahi kuwa na nia ya kumiliki silaha za nyuklia na kwamba kushikamana kwa Iran na makubaliano ya NPT kuko wazi kwa kila mtu.
(last modified 2025-01-23T10:35:14+00:00 )
Jan 23, 2025 10:35 UTC
  • Sayyid Abbas Araqchi
    Sayyid Abbas Araqchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amejibu matamshi yaliyotolewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres akisisitiza kuwa Iran haijawahi kuwa na nia ya kumiliki silaha za nyuklia na kwamba kushikamana kwa Iran na makubaliano ya NPT kuko wazi kwa kila mtu.

Sayyid Abbas Araqchi aliyasema hayo akijibu matamshi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres dhidi ya Iran katika kikao cha Jumatano cha Davos.

Mapema leo Alhamisi, Araqchi ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Ni utovu wa adabu na haya kuwahubiria Wairani. Waweke wazi mara moja na daima kwamba wataacha madai kuwa (Iran) ina silaha za nyuklia."

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza zaidi kuwa: "Kujitolea kwa muda mrefu kwa Iran kwa mfumo wa kimataifa wa kutoeneza silaha za maangamizi kuko wazi kwa kila mtu."

Amekumbusha kwamba "Iran ilitia saini mkataba wa NPT mwaka 1968 kama mmoja wa wanachama waasisi," na kuiandika kuwa: "Kiongozi Mkuu wa Iran ametangaza kuwa silaha zote za maangamizi ya wanadamu ni haramu, kwa kutoa amri ya kidini."

Araqchi pia ameandika: Mwaka 2015, Iran ilitia saini mapatano ya nyuklia ya JCPOA ambayo yaliweka mfumo mkubwa zaidi wa ukaguzi katika historia ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kusema kwa uwazi: Iran kwa mara nyingine tena inasisitiza kwamba, kwa hali yoyote ile, haina nia ya kumiliki au kuzalisha silaha za nyuklia.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Swali muhimu zaidi" katika eneo letu ni mauaji ya kimbari ya Israel huko Gaza na kukalia kwa mabavu maeneo ya Palestina, Syria na Lebanon. Ni kuhusu silaha za nyuklia ya Israel na kukataa kujiunga utawala huo na NPT ambako ni tishio kwa ulimwengu. Ukweli huu haupaswi kupuuzwa au kufumbiwa macho."

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, alisema jana Jumatano katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia huko Davos, Uswisi, kwamba Iran inapaswa kuchukua hatua ya kwanza ya kuboresha uhusiano na nchi za kikanda na Marekani kwa kuweka wazi kwamba lengo lake si kuzalisha silaha za nyuklia.