Meja Jenerali Salami: Ushindi wa Gaza unamaanisha ushindi kwa ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121848-meja_jenerali_salami_ushindi_wa_gaza_unamaanisha_ushindi_kwa_ulimwengu_wa_kiislamu
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SPAH) amesema kuwa, kujiuzulu kwa maafisa wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kumalizika vita vya Gaza ni ishara tosha ya kushindwa kwao katika vita vya Gaza.
(last modified 2025-01-24T05:49:57+00:00 )
Jan 24, 2025 05:49 UTC
  • Meja Jenerali Salami: Ushindi wa Gaza unamaanisha ushindi kwa ulimwengu wa Kiislamu

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SPAH) amesema kuwa, kujiuzulu kwa maafisa wa kijeshi wa utawala wa Kizayuni wa Israel baada ya kumalizika vita vya Gaza ni ishara tosha ya kushindwa kwao katika vita vya Gaza.

Meja Jenerali Hossein Salami amebainisha kwamba, kama Gaza ingeshindwa, Uislamu ungedhurika na kupata pigo na kutokana na kuwa Gaza imeshinda basi hii ina maana kwamba, Uislamu umepata ushindi.

Sambamba na kuashiria engo za ushindi wa Harakati ya Hamas na Jihadul-Islami dhidi ya adui Mzayuni licha ya kuangamizwa kidhahiri Gaza na njaa na kiu ya wananchi wa Palestina, amesema: Ardhi sio mahali ambapo makafiri wanawashinda waumini, hata kama waumini wote watauawa shahidi, na tuliona mfano wa hili katika tukio kubwa la Karbala. Wale waliosimama kidete na mioyo  imara na thabiti walishinda katika uwanja wa Gaza, huku nyoyo ikivunjika katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel.

Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (SEPAH) ameongeza kusema kuwa, Marekani, utawala haramu wa Israel na Uingereza ziliungana kuvunja taifa lisilo na ulinzi, lakini taifa la Palestina lilisimama kwa adhama na kuibuka na ushindi.

Kadhalika Meja Jenerali Salami amesema, matukio ya hivi karibuni yameonyesha kuwa damu imepata ushindi dhidi ya upanga na wananchi wa Palestina wameibuka na ushindi katika vita dhidi ya Wazayuni.