Rais wa Iraq: Iran ni jirani mkubwa na muhimu kwa Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i121900-rais_wa_iraq_iran_ni_jirani_mkubwa_na_muhimu_kwa_iraq
Rais wa Iraq amesema kuwa, Iran ni jirani mkubwa na muhimu kwa Iraq na kubainisha kwamba, uhusiano kati ya Baghdad na Tehran ni wa kawaida na wa kirafiki.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 25, 2025 22:52 UTC
  • Rais wa Iraq: Iran ni jirani mkubwa na muhimu kwa Iraq

Rais wa Iraq amesema kuwa, Iran ni jirani mkubwa na muhimu kwa Iraq na kubainisha kwamba, uhusiano kati ya Baghdad na Tehran ni wa kawaida na wa kirafiki.

Akijibu swali la mwandishi wa Bloomberg kuhusu jinsi anavyotathmini uwepo wa Iran nchini Iraq, Rais Abdul Latif Rashid alisema: Iran ni jirani mkubwa na muhimu kwa Iraq. Wairani na Wairaki wana historia kongwe ya maingiliano na kuishi pamoja.

Rais Abdul Latif Rashid amesema: Kwa kuzingatia ukweli na uhalisia huo, Iraq haiwezi kuipuuza Iran, kama ambavyo Iran nayo haiwezi kufanya hivyo.

Ameongeza kuwa, watu wa Iran na Iraq wana uhusiano wa kijamii, kidini na hata kifamilia. Daima kumemekuweko na uhusiano kati ya watu, kibiashara na mazungumzo kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Iraq aliongeza kuwa, Iraq ni nchi huru. Nina furaha kutangaza kwamba uhusiano wetu na Iran ni wa kawaida na wa kirafiki. Pia nataka kusisitiza kwamba hatutaruhusu nchi yoyote kuingilia maamuzi yetu.

Alisema: "Kwa bahati mbaya, vikosi vya Uturuki katika eneo la Kurdistan vinaendelea kuingilia masuala yetu na tunaiomba Uturuki kukomesha uingiliaji huo." Hatutaruhusu nchi yoyote kudhoofisha uhuru wetu. Pia, hatutaruhusu shambulio lolote kutoka eneo la Iraq hadi nchi jirani.