Uhusiano wa kibiashara wa Iran na Oman wazidi kustawi
Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran ametangaza habari ya kuzidi kustawi na kuimarika uhusiano wa kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Oman.
Abbas Aliabadi amesema hayo na kuongeza kuwa, baada ya kutiwa saini hati ya ushirikiano baina ya Iran na Oman katika mkutano wa 21 wa Kamisheni ya Pamoja ya Ushirikiano wa nchi hizo mbili, sasa mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi hizi mbili ndugu na rafiki yanakadiriwa kuwa yatafika takriban dola bilioni 5 kwa mwaka.
Kwa mujibu wa takwimu za forodha, biashara baina ya Iran na Oman ilifikia takriban dola bilioni mbili na nusu mwaka jana, na katika kipindi cha miezi saba iliyopita, mauzo ya bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa jirani yake ya kusini yaani Oman yalifikia takriban dola bilioni moja.
Uhusiano kati ya Iran na Oman katika miongo ya hivi karibuni daima umekuwa juu ya msingi wa kuheshimiana na kulindwa maslahi ya pande zote, licha ya kuweko mivutano katika eneo la Ghuba ya Uajemi na njama za Marekani za kueneza chuki dhidi ya Iran.
Viongozi wa Oman wanaamini kuwa, uhusiano wao wa karibu na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unazingatia uhalisia wa mambo na wanaichukulia Iran kuwa ni jirani yake muhimu na mkubwa.
Nchi hizo mbili hazina mizozo ya kieneo na wala ya mipaka kati yao. Daima Iran inaunga mkono misimamo ya Oman, kama ambavyo Muscat nayo haingilii misimamo na mambo ya ndani ya Iran.