Salami: IRGC ina 'Akili Mnemba' ya kutumia kwenye operesheni ngumu za kijeshi
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema kikosi cha wasomi cha jeshi hilo la Iran kimejizatiti kwa teknolojia ya Akili Mnemba ili kutekeleza vyema operesheni nzito na ngumu za kijeshi.
Akihutubia mkutano wa kimataifa wa Akili Mnemba (Artificial Intelligence) hapa mjini Tehran, Kamanda Mkuu wa IRGC, Meja Jenerali Hossein Salami amesema kuielewa na kuitumia Akili Mnemba ni muhimu kwenye operesheni za kisasa za kijeshi.
Amesisitiza kuwa, Akili Mashine inaweza kuimarisha operesheni za kijeshi. Kwa mfano, amebainisha kuwa manowari ya maadui inapogunduliwa, teknolojia ya Artificial Intelligence inaweza kusaidia kutambua shabaha mahususi kwenye meli hiyo, na kuwezesha kupigwa kwa usahihi huku ikihakikisha usalama wa mabaharia wa chombo hicho.
Kamanda Salami ameeleza bayana kuwa, "Teknolojia ya hali ya juu ya AI inatuwezesha kupata meli tunayotaka kwa kutumia teknolojia ya mlinganisho wa picha." Salami aidha amesema ndege zisizo na rubani zinaweza kupiga meli kubwa za adui bila kusababisha uharibifu mkubwa.
Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu pia amegusia jukumu la Akili Mnemba katika ulinzi wa anga. Amesema kufanya mashambulizi kadhaa kwa wakati mmoja kwa kutumia ndege nyingi kunaweza kuelemea maamuzi ya binadamu. Anasisitiza kuwa, Akili Bandia inaweza kutoa suluhisho la haraka katika hali kama hizi.
Mbali na kutumiwa katika masuala ya kijeshi, Jenerali Salami amesema Akili Mnemba inaweza kutumiwa katika sekta zingine kama vile huduma za afya, shughuli za uokoaji, usafiri wa anga na usafirishaji.