Mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran kikanda na duniani
Leo Iran inaadhimisha miaka 46 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotokea mwaka 1979 chini ya uongozi wa hayati Imam Ruhullah Khomeini. Matokeo na mafanikio ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran daima yamekuwa na taathira kwa kanda ya Asia Magharibi na dunia kwa ujumla.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yanahesabiwa kuwa mapinduzi muhimu na makubwa zaidi katika nusu ya pili ya karne ya ishirini. Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, kwa hakika, ilikuwa kutimia irada na matakwa ya taifa kubwa ya kupata uhuru na kujitawala, izza na utu na kuondoka chini ya udhibiti wa madola ya kibeberu. Kipindi hicho ambapo dunia iligawanyika baina ya madola mawili makubwa ya Mashariki na Magharibi, Mapinduzi ya Kiislamu ya wananchi wa Iran yalipata ushindi na kuuangusha utawala kibaraka na tegemezi kwa Magharibi wa Shah Pahlavi kwa kaulimbiu ya "Si Mashariki wala Magharibi" chini ya uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini.
Siku ya leo ya tarehe 22 Bahman siku ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kumbukumbu ya moja ya matukio makubwa ya kihistoria ya taifa kubwa la Iran. Kila mwaka, mamilioni ya watu kote ndani ya Iran ya Kiislamu hushiriki katika maandamano makubwa ya kuadhimisha siku hii na kutangaza tena utiifu wao kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi hayo.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulisababisha mabadiliko makubwa katika hatima ya taifa la Iran na kuibua fikra mpya za kimapinduzi zenye kuegemea kwenye mafundisho ya Mwenyezi Mungu katika mapambano ya mataifa dhidi ya mfumo wa kibeberu. Kwa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, taifa la Iran lilijikomboa kutoka kwenye utegemezi mbaya wa kihistoria na kutawaliwa kwa fedheha na madola ya kibeberu na kuingia kwenye njia ya uhuru, kujitawala, utu na maendeleo katika nyanja zote. Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia yalikuwa na taathira kubwa kwa mataifa yaliyokuwa yakidhulumiwa na kukandamizwa duniani na yamesababisha mageuzi makubwa katika mwamko wa Kiislamu na kuanzisha safu ya muqawama na mapambano dhidi ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Mshikamano wa wananchi na Mapinduzi ya Kiislamu ambao utadhihirika tena leo unaonyesha kwamba, wananchi wa Iran wanaelekea kwenye mustakbali mwema licha ya njama zote zinazofanywa na maadui. Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa mfano wa kuigwa sio tu kwa taifa la Iran na Waislamu katika nchi nyingine, bali pia kwa watu wanaopigania uhuru na kujitawala duniani kote. Kwa hivyo, maandamano makubwa ya mwaka huu hapa nchini pia ni ukumbusho wa maadili na malengo ya juu ya Mapinduzi na ujenzi wa ustaarabu mpya wa Kiislamu kwa Waislamu wote na wapenda uhuru dunia.
Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran tarehe 11 Februari 1979 unahesabiwa kuwa mabadiliko makubwa katika historia ya maelfu ya miaka ya Iran. Mapinduzi haya yamesababisha mabadiliko ya kimsingi katika maeneo mbalimbali ya jamii ya Iran yakiwemo mabadiliko ya kisiasa, kijamii, kiutamaduni na kiuchumi.

Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalifungua upeo mpya wa umoja wa Umma wa Kiislamu na mapambano dhidi ya ubeberu wa kimataifa unaoongozwa na Marekani, kwa kuwasilisha ujumbe mpya na kuunda kituo cha kuwatetea watu wanaodhulumiwa na wanaopigania kujitawala, mbele ya macho ya zaidi ya Waislamu bilioni moja, na kuzua wimbi la hofu katika nyoyo za madola ya kibeberu.
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia yamekuwa kigezo chenye mafanikio na taathira katika Ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na sera za kupenda kujitanua na kuhodhi kila kitu za Marekani na nchi za Magharibi kwa ujumla, na yamewafanya Waislamu duniani kote wajiamini hasa kuhusu umuhimu na hadhi ya thamani za kidini na kimaadili.

Moja ya mafanikio muhimu ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia ni kuunda utambulisho madhubuti na wa kipekee wa Mhimili wa Muqawama wa Kiislamu. Ushindi huo wa Mapinduzi ya Kiislamu ulisambaratisha milinganyo yote kati ya Mashariki na Magharibi na kulirudisha tena kwenye macho na mazingatio ya walimwengu suala la mapambano ya ukombozi wa Palestina ambalo lilikuwa likikaribia kusahaulika.