Je, unaujua mtazamo wa Iran kuhusu uhusiano na nchi za Afrika?
Mohammad Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika kikao na wakuu wa balozi za nchi za Afrika zilizopo mjini Tehran kwamba: Kukuza uhusiano wa kiuchumi na kibiashara na bara la Afrika ni moja ya vipaumbele vya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu nchi za Afrika ni mtazamo unaozingatia kustawisha mahusiano katika nyanja mbalimbali, ikiwa ni pamoja na uwanja wa kiuchumi. Bara la Afrika linajulikana kama bara la fursa, lenye uwezo wa kibiashara wa dola bilioni 600. Uhusiano wa Iran na Afrika katika miaka ya hivi karibuni umejikita zaidi katika masuala ya kilimo, madini na dawa. Kwa kuongezea ni kuwa, bidhaa za teknolojia za makampuni ya Iran ambayo msingi wake ni elimu, pia zimepata wateja wengi katika nchi za Afrika. Lakini hadi hivi sasa Iran inafaidika na asilimia moja tu ya soko la Afrika. Hivi sasa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inachukua hatua mbalimbali za kuhakikisha inakuwa na nafasi kubwa zaidi katika uchumi na nchi za Afrika.
Ni kwa sababu hiyo ndio maana Mohammad Reza Aref, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran akasema: "Kukuza kwa kiwango cha juu ushirikiano wa Iran na bara la Afrika katika msingi wa kuheshimiana pande mbili, pande nyingi na uhusiano wa kimataifa katika ajenda tofauti." Gholamreza Nouri, Waziri wa Jihadi ya Kilimo wa Iran kwa upande wake alisema katika kikao na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sudan, Ali Youssef Ahmed Al-Sharif hapa mjini Tehran kwamba: "Iran iko tayari kuwapa watafiti wa Sudan matokeo ya utafiti wake wa miaka mia moja katika uzalishaji wa mimea na mifugo."
Mbali na uhusiano wa kiuchumi, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia inaendeleza ajenda yake ya kustawisha uhusiano na nchi za Afrika katika nyanja nyinginezo zikiwemo za kisiasa. Kwa kuzingatia misimamo ya nchi za Afrika ya kuchukia ukoloni, kuchukia jinai za Uzayuni na kuchukia ubaguzi wa rangi, Iran inaona kwamba kuna nafasi pia ya kupanua uhusiano wa kisiasa kati ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Afrika. Afrika Kusini ndiye mpeperushaji bendera ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel barani Afrika. Afrika Kusini imekuwa na nafasi kubwa katika kutolewa hukumu za kutiwa mbaroni viongozi wa Israel kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kutokana na jinai zao za kivita huko Ghaza, Palestina. Kwa hivyo, kuna mambo mengi yanayofanana kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na nchi za Afrika.
Wakati huo huo, idadi kubwa ya nchi za Afrika pia zina matatizo ya ukosefu wa usalama na vitisho vya kigaidi. Kwa kuzingatia uzoefu mkubwa ambao Jamhuri ya Kiislamu imepata katika kupambana na ugaidi na magenge ya ukufurishaji, Iran inaweza kuzisaidia nchi za Afrika kupambana na mambo hayo yanayohatarisha usalama wa nchi hizo. Nchi za Afrika pia zimekuwa zikionesha hamu ya kunufaika na uzoefu wa Iran katika kupambana na ugaidi wakati wa mkutano wao na maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kiujumla ni kwamba, azma ya kweli ya pande mbili na nia ya kweli ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kuendeleza uhusiano na nchi za Afrika kwa msingi wa kuheshimiana, utu na ubinadamu sambamba na kuzingatia maslahi ya pamoja, kumezifanya nchi za Afrika kukaribisha upanuzi wa uhusiano na hata kuikubali Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Afrika.
"Ismail Baghaei Hamaneh," Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ikiwa ni mwanachama mwangalizi wa Umoja wa Afrika, iko tayari kuimarisha uhusiano na kupanua ushirikiano na nchi za Afrika katika nyanja mbalimbali za maslahi ya pande zote."