Kamanda Irani: Nchi za kanda zinaweza kujidhaminia usalama
(last modified Wed, 12 Mar 2025 12:43:47 GMT )
Mar 12, 2025 12:43 UTC
  • Kamanda Irani: Nchi za kanda zinaweza kujidhaminia usalama

Kamanda wa Jeshi la Wanamaji wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa maadui wanapaswa kubadili mtazamo wao kuhusu kanda hii na kusisitiza kuwa nchi za kanda zinaweza kuhakikisha usalama wao wenyewe.

Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ameyasema hayo katika majojiano na televisheni  Al Jazeera, na kuongeza kuwa ukosefu wowote wa usalama na uthabiti katika kanda hii huathiri uchumi wa dunia. Amesisitiza kuwa madhumuni ya mazoezi ya kijeshi ya Jeshi la Wanamaji ni kuhakikisha usalama na uthabiti katika eneo hilo.

Admeri Irani almengeza kuwa mazoezi ya Jeshi la Wanamaji, hasa katika hali ya sasa ya kanda, yanafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa. Alisema kuwa ujumbe wa Mazoezi ya Pamoja ya "Ukanda wa Usalama wa Baharini 2025" kwa maadui ni kwamba Iran haijatenwa.

Mazoezi haya ya saba ya "Ukanda wa Usalama wa Baharini 2025" yalianza Jumatatu, Machi 10, yakihusisha vikosi vya majini vya Russia na China, pamoja na nchi waangalizi ambazo ni Jamhuri ya Azerbaijan, Afrika Kusini, Oman, Kazakhstan, Pakistan, Qatar, Iraq, Falme za Kiarabu, na Sri Lanka.  Mazoezi hayo yanayojumuisha Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) yanafanyika katika eneo la kaskazini mwa Bahari ya Hindi.

Meli ya kivita ya Iran ikiwa katika mazoezi

Mazoezi haya yanafanyika kwa lengo la kuboresha usalama, ushirikiano endelevu wa usafiri wa baharini, na uhusiano kati ya Jeshi la Wanamaji la Iran, Jeshi la Wanamaji la China, na Jeshi la Wanamaji la Russia katika kupanga na kutekeleza operesheni za pamoja za baharini.

Wakati huo huo,Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesisitiza kuwa, mazoezi  hayo ya pamoja ya kijeshi yanadhihirisha ushujaa na uwezo mkubwa wa Jeshi la Wanamaji la Jamhuri ya Kiislamu katika medani za kimataifa.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran ameeleza azma ya Jamhuri ya Kiislamu ya kudumisha na kuimarisha usalama wa Ghuba ya Uajemi, Lango-Bahari la Kistratijia la Hormuz, Bahari ya Oman na kwingineko, na amesisitiza kwamba maneva ya hivi sasa yatadhihirisha azma hiyo mbele ya waangalizi wa kimataifa.